Iran: Wapalestina wataamua hatima yao wenyewe
(last modified Mon, 27 Nov 2023 11:26:14 GMT )
Nov 27, 2023 11:26 UTC
  • Iran: Wapalestina wataamua hatima yao wenyewe

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema taifa la Palestina halitaruhusu ama utawala wa Kizayuni au Marekani kufikia malengo yao haramu, na kusisitiza kuwa hatima ya Palestina ipo mikononi mwa Wapalestina wenyewe.

Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema hayo leo katika kikao cha kila wiki na waandishi wa habari hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, Marekani imekuwa sehemu ya matatizo ya Wapalestina kwa miaka mingi.

Amesema Marekani ni mshirika wa Israel katika uvamizi na mashambulizi ya siku 48 ya utawala huo pandikizi dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi wa Ukanda wa Gaza.

Vita vya mauaji ya kimbari vya utawala katili wa Israel dhidi ya Gaza vimesababisha vifo vya takriban Wapalestina 15,000, wengi wakiwa ni wanawake na watoto.

Kan'ani amebanisha kuwa, iwapo Marekani haingeliunga mkono utawala haramu wa Israel, basi vita vya Gaza visingelitokea. Amesema, "Uungaji mkono wa kisiasa wa Washington katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na wa kijeshi katika eneo ulipelekea vita hivyo visisimamishwe ndani ya muda mfupi."

Amekumbusha kuwa leo ndiyo siku ya mwisho ya muda wa usitishaji vita wa kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, na kwamba Iran inataraji kuwa jinai za utawala wa Kizayuni hazitakaririwa katika eneo hilo, na usitishaji vita huo utakuwa endelevu na wa kudumu.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amefichua kuwa, nchi 120 duniani zinaunga mkono kuendelea kutekelezwa usitishaji vita huo kwa misingi ya binadamu katika Ukanda wa Gaza.

"Takwa la jamii ya kimataifa liko wazi, uvamizi na mashambulizi ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza yanapasa kukomeshwa," ameongeza Kan'ani.