Rais wa Iran asusia mkutano wa COP28 Dubai kwa kushiriki Israel
(last modified Fri, 01 Dec 2023 06:47:36 GMT )
Dec 01, 2023 06:47 UTC
  • Rais wa Iran asusia mkutano wa COP28 Dubai kwa kushiriki Israel

Rais Ebrahim Raisi wa Iran hatashiriki mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28, mjini Dubai kutokana na uwepo wa Rais Isaac Herzog na maafisa wengine wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye mkutano huo.

Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo na kueleza kuwa: Kutokana na mualiko kwa maafisa wa utawala wa Kizayuni kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hatashiriki mkutano huo.

Badala yake, Iran imemtuma Ali Akbar Mehrabian, Waziri wa Nishati wa Jamhuri ya Kiislamu kwenda kwenye mkutano huo kubainisha msimamo na mapendekezo ya Iran juu ya namna ya kukabiliana na uchafuzi wa hewa.

Mapema jana, Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Imarati, Sheikh Abdullah bin Zayed Al Nahyan, alimshukuru Rais wa UAE kwa kumualika Rais wa Iran kwenye mkutano huo, lakini akamfahamisha kuwa Sayyid Raisi hatouhudhuria kutokana na uwepo wa maafisa wa Kizayuni.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Imarati alimkabidhi Abdollahian mualiko huo wa kumuomba Sayyid Raisi ashiriki mkutano huo wakati wa kongamano la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Marafiki wa BRICS mjini Cape Town nchini Afrika Kusini mwezi Juni.

Viongozi kutoka nchi zaidi ya 100 duniani wanahudhuria mkutano huo wa 28 wa kujadili taathira hasi za mabadiliko ya tabianchi, ulioanza jana Alkhamisi mjini Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu.

Rais Ebrahim Raisi wa Iran amekuwa akisisitiza kuwa, Israel imefeli kufikia malengo yake yote katika hujuma na mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya wananchi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza, na kwamba Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa ni jibu halali la taifa la Palestina, mkabala wa dhulma za muda mrefu za utawala ghasibu wa Israel.

Tags