Droni za Karrar zilizoboreshwa zajiunga na Kikosi cha Anga cha Iran
Makumi ya ndege zisizo na rubani (droni) aina ya Karrar ambazo zimeboreshwa na kuimarishwa zimejiunga na Kikosi cha Ulinzi wa Anga cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Droni hizo zilizoundwa na wataalamu wa hapa nchini zimezinduliwa leo Jumapili katika hafla iliyofanyika katika Chuo cha Ulinzi wa Anga cha Khatam Al-Anbia hapa mjini Tehran, mbele ya makamanda na maafisa wa ngazi za juu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Iran.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Press TV, droni za Karrar zimesimikwa makombora ya angani hadi angani ya Majid, na zina uwezo mkubwa wa kukabliana na chombo chochote cha angani cha adui kwa usahihi mkubwa.
Droni hizo zilifanyiwa majaribio kwa mafanikio wakati wa luteka ya kijeshi ya ndege zisizo na rubani za Iran mnamo mwezi Oktoba mwaka huu.
Droni ya Karrar, iliyotengenezwa na Kampuni ya Viwanda ya Kutengeneza Ndege ya Iran (HESA), ni miongoni mwa kizazi kipya cha zana za anga za Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu iliyoundwa kuzuia vyombo vinavyoruka vya maadui kuingia katika anga ya Iran.
Akizungumza katika hafla ya kuzinduliwa droni hizo hii leo, Meja Jenerali Abdolrahim Mousavi, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran ameashiria nguvu ya ndege zisizo na rubani za jeshi la Iran zinavyoongezeka kwa idadi na ubora na kusema: Maadui wanapinga uwezo wa Iran, na uzoefu umethibitisha kuwa nguvu zetu zinawatia kiwekwe na kuwakatisha tamaa maadui.
Amesisitiza kuwa ndege zisizo na rubani zina nafasi kubwa katika vita na kwamba kuwepo aina tofauti za ndege hizo hapa nchini kunaongeza uwezo wa makamanda kufanya maamuzi katika medani ya vita.
Naye Brigedia Jenerali Alireza Sabahifard, Kamanda wa Kikosi cha Ulinzi wa Anga cha Iran amesema, "Droni ya Karrar ni mafanikio makubwa ya vijana wa taifa hili."