Kamanda wa IRGC: Israel itakabiliwa na jibu lisilofikirika
(last modified Fri, 01 Nov 2024 10:32:29 GMT )
Nov 01, 2024 10:32 UTC
  • Kamanda wa IRGC: Israel itakabiliwa na jibu lisilofikirika

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) ameionya Israel kwamba, itapata jibu kali na zito kwa kitendo chake cha hivi karibuni cha uchokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu; jibu ambalo halifikiriki wala kutasawirika.

Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda wa IRGC ametoa onyo hilo leo Ijumaa katika Kongamano la Pili la Kitaifa la Mashahidi 15,000 wa mkoa wa Fars na kuongeza kuwa: Waisraeli wanafikiri wanaweza kubadilisha historia kwa kurusha makombora machache tu (dhidi ya Iran).

Meja Jenerali Salami ameuhutubu utawala huo wa Kizayuni kwa kuuambia: Hamjasahau Operesheni ya Ahadi ya Kweli ya 2, mlifeli (kuzima wimbi la makombora ya Iran), (iwapo hamkujifunza) mjue kuwa tutatoa jibu (kali zaidi) lisiloweza kufikirika.

Kamanda Mkuu wa jeshi la SEPAH la Iran ameongeza kuwa: Israel ipo katika ukingo wa kuporomoka, na ndiposa katika siku za karibuni inafanya jinai kwa upofu na bila ya kanuni zozote.

Iran: Jibu kali na zito linaisubiri Israel

Ameuonya utawala wa Kizayun kuwa, "Tunawaonya na kuwataka warejelee (kumbukumbu za) historia. Tazama historia ya miaka 45 iliyopita na mielekeo ya Iran kwa maadui zake; Umechagua njia ya kuporomoka na umepoteza uhai wake wote, lakini bado haujifunzi kutoka kwa historia."

Indhari hiyo ya Kamanda Mkuu wa IRGC imekuja wiki moja baada ya Israel kufanya shambulio la kichokozi dhidi ya vituo vya kijeshi vya Iran; chokochoko ambazo Jamhuri ya Kiislamu mbali na kufanikiwa kulizima kwa mafanikio, lakini imeapa kulijibu.