Mauaji ya umati ya Wapalestina kwa silaha za Marekani
Kuendelea jinai za utawala wa Kizayuni huko Ghaza kwa kutumiwa silaha za Marekani limekuwa suala lenye utata linalojadiliwa katika duru za kisiasa na vyombo vya habari vya Marekani.
Gazeti la The Washington Post limeandika katika ripoti yake kuhusiana na hilo kuwa: "Nyaraka za jinai zinazofanywa na Israel kwa kutumia silaha za Marekani ni nyingi mno kiasi kwamba lau Washington ingekuwa na dhamira ndogo tu ya kukabiliana na jinai hizo, ingeifanya Israel iwajibike kimataifa."
Kwa mujibu wa gazeti la Washington Post, Marekani imepokea karibu ripoti 500 kwamba Israel inatumia silaha za Marekani kushambulia raia wa kawaida katika Ukanda wa Gaza. Hata hivyo, Washington imekiuka sheria za kimataifa na sera zake ilizozitangaza yenyewe na kuamua kutoiwajibisha Israel.
Afisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ambaye alijiuzulu kufuatia serikali ya nchi hiyo kutochukua hatua zozote dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni ameliambia gazeti la Washington Post kwamba, maafisa wa nchi hii wanapochunguza ripoti za jinai za Wazayuni hujaribu kutafuta njia za kuficha ukweli na kuhafifisha jinai hizo mbele ya macho ya walimwengu.
Tangu kukaliwa kwa mabavu Palestina na kuasisiwa utawala bandia wa Israel, utawala huo ghasibu ndio umekuwa kituo cha kupokea misaada ya nje ya Marekani, ukipokea dola bilioni 310 za misaada ya kiuchumi na kijeshi. Kupitia mkataba wa maelewano, Marekani imeahidi kutoa dola bilioni 3.8 kwa Israeli kila mwaka hadi 2028, misaada ambayo huongezwa maradufu wakati wa vita. Tangu Israel ilipovamia Gaza mwezi Oktoba mwaka jana, Marekani imetoa msaada wa kifedha wa zaidi ya dola bilioni 22 kwa utawala wa Israel.
Taasisi ya Watson ya Chuo Kikuu cha Brown cha Marekani pia imechapisha ripoti hivi karibuni na kusema kwamba serikali ya Biden imelipa asilimia 70 ya gharama za vita huko Gaza. Katika sehemu nyingine ya ripoti yake, chombo hiki cha wanafikra kimesema kuendelea vita vya Israel huko Gaza kunatokana na msaada wa kifedha wa Marekani na kuandika: "Hapana shaka kwamba bila ya misaada ya Marekani, nakisi ya bajeti ya Israel ingefikia kiwango kisichokuwa na mfano wake kati ya mwaka 2024 na 2025, hivyo ni wazi kuwa vita hivi haviwezi kuendelea kwa nguvu na upeo wake wa sasa bila ya misaada ya Marekani."
Sambamba na misaada hiyo, Marekani pia inatoa uungaji mkono mkubwa wa kisiasa kwa utawala wa Kizayuni. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Ikulu ya White House imezuia kupitishwa azimio lolote katika Baraza la Usalama ambalo linaukosoa utawala wa Kizayuni au kutoa mashinikizo dhidi ya utawala huo. Theluthi mbili ya maazimio yaliyopigiwa kura ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tangu umoja huo uasisiwe, yanahusiana na utawala wa Kizayuni, na yote yalipigiwa kura ya turufu na Marekani.
Licha ya kuwa uungaji mkono wa pande zote wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni sio siri tena, lakini kiwango cha jinai zinazofanywa na Wazayuni huko Ghaza ni kikubwa na cha kutisha kiasi kwamba, uungaji mkono huo wa Marekani kwa Wazayuni wanaokalia kwa mabavu Quds Tukufu, sasa umevuka mpaka na kuvijumuisha pamoja vyama vyote viwili vya Democratic na Republican. Hivi sasa mjadala huu unajadiliwa katika ngazi za kisiasa, vyombo vya habari na kitaaluma, kwamba uungaji mkono mkubwa na wa kila upande wa Marekani kwa Wazayuni umehatarisha nafasi ya Marekani katika eneo zima la Asia Magharibi. Israel, kama mwanaharamu wa Marekani, haiwezi tena kudhamini maslahi ya Marekani katika eneo, na jinai zilizokithiri za Wazayuni pia zinahusishwa na Marekani.
Ukweli wa mambo ni kwamba utawala bandia wa Israel hauna uwezo wa kukabiliana kijeshi na makundi ya muqawama katika eneo hili bila ya uungaji mkono wa Marekani. Katika upande wa pili, kuendelea muqawama wa wananchi wa Palestina kunaonyesha kuwa hakuna silaha yoyote iliyo na uwezo wa kushinda dhamira na muqawama wa taifa linalodhulumiwa chini ya utawala vamizi.