Mauritius yazuia upatikanaji huduma za mitandao ya kijamii
(last modified Sat, 02 Nov 2024 02:56:39 GMT )
Nov 02, 2024 02:56 UTC
  • Mauritius yazuia upatikanaji huduma za mitandao ya kijamii

Mauritius imezuia huduma za mitandao ya kijamii, siku chache tu kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu.

Hatua hiyo imechuukuliwa huku mvutano ukiongezeka kuhusu kashfa ya kuvujisha mawasiliano ya simu.

Uamuzi huo wa kushtusha umetangazwa na kampuni ya simu EMTEL, ambayo imesema imeamriwa na Mamlaka ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kuzuia huduma za majukwaa yote ya mitandao ya kijamii. Hatua hiyo inatarajiwa kudumu hadi Novemba 11 siku moja baada ya uchaguzi.

Ofisi ya Waziri Mkuu imesema kanda za sauti zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii katika wiki mbili zilizopita huenda zilihatarisha usalama wa nchi hiyo ya kisiwa cha Bahari Hindi.

Mawasiliano hayo yaliwahusisha wanasiasa, polisi, wanasheria, waandishi habari, wanachama wa mashirika ya kijamii yalivujishwa tangu katikati ya Oktoba. Waziri Mkuu Pravind Kumar Jugnauth anatafuta muhula mwingine kama mkuu wa chama cha Militant Socialist Movement. Alirithi uwaziri mkuu kufuatia kifo cha babake mwaka wa 2017 na akaupa ushindi muungano wake katika uchaguzi miaka miwili baadaye.