Zambia yapinga matakwa ya Marekani yanayohusiana na mkataba wa afya na madini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i138282-zambia_yapinga_matakwa_ya_marekani_yanayohusiana_na_mkataba_wa_afya_na_madini
Zambia imeishutumu hadharani Marekani kwa kuunganisha kifurushi cha afya kilichopendekezwa cha dola bilioni 2 na matakwa kupewa data na madini na muhimu, ikisema baadhi ya masharti yaliyoambatanishwa na makubaliano hayo "hayakubaliki".
(last modified 2026-05-10T10:28:39+00:00 )
May 10, 2026 10:24 UTC
  • Mulambo Haimbe, Waziri wa Mambo ya Nje wa Zambia
    Mulambo Haimbe, Waziri wa Mambo ya Nje wa Zambia

Zambia imeishutumu hadharani Marekani kwa kuunganisha kifurushi cha afya kilichopendekezwa cha dola bilioni 2 na matakwa kupewa data na madini na muhimu, ikisema baadhi ya masharti yaliyoambatanishwa na makubaliano hayo "hayakubaliki".

Akieleza kwa mara ya kwanza sababu ya kukwama mazungumzo kuhusu makubaliano ya afya yanayofadhiliwa na Marekani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Zambia, Mulambo Haimbe amesema serikali ilikataa kukubali sehemu za mkataba uliopendekezwa kwa sababu Wamarekani walijumuisha humo matakwa ka kupewa data ya raia na upendeleo kwa makampuni ya madini ya Marekani.

"Kutoa data za watu (kwa nchi nyingine) ni ukiukaji wa haki ya faragha ya raia wetu. Masuala haya yanashughulikiwa katika mahakama za Zambia na hili lazima liheshimiwe," amesema Haimbe katika hotuba iliyorushwa hewani kwenye televisheni.

Haimbe pia amesema Zambia ilipinga juhudi za kuunganisha mazungumzo ya afya na makubaliano tofauti ya madini muhimu. Amesema serikali ya Luusaka ilikuwa na wasiwasi kwamba Marekani ilitaka makubaliano hayo mawili yachukuliwe kama sehemu ya kitu kimoja.

Wanaharakati wa afya pia wamekosoa majaribio ya kuunganisha ufadhili wa huduma ya afya na upatikanaji wa madini ya kimkakati. "Wakati afya za watu zinapofanywa wenza ya kujadili bei ya bidhaa, afya za watu zinakuwa jambo dogo na lisilo na maana," amesema Asia Russell, mkurugenzi mtendaji wa kundi la Health GAP.

Waziri Haimbe amesema Zambia inasisitiza kwamba makubaliano hayo mawili lazima yatambuliwe kuwa tofauti.

Zambia ni mzalishaji wa pili kwa ukubwa wa shaba barani Afrika baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Pia ina akiba kubwa ya kobalti, nikeli, manganese, grafiti, lithiamu na elementi adimu za ardhini.