Ongezeko la vifo kabla ya Hija laibua taharuki nchini Saudi Arabia
-
Makka, Saudi Arabia
Ripoti za kuongezeka vifo baina ya mahujaji waliokwenda Saudi Arabia kutekeleza ibada ya Hija kumezua wasiwasi na taharuki baina ya viongozi na wasimamizi wa ibada hiyo.
Wasaudia wanasisitiza kwamba ongezeko la vifo halina uhusiano wowote na virusi, lakini sasa kwa kuwa zimesalia wiki mbili tu kabla ya kuanza ibada ya Hija, wanafikiria kuimarisha na kuongeza idadi ya timu za matibabu.
Mahujaji 23 kutoka nchi nne wamefariki dunia nchini Saudi Arabia katika siku zilizotangulia kuanza msimu wa Hija wa 2026. Ikithibitisha takwimu hizo, Wizara ya Afya ya Saudi Arabia imetangaza kwamba "hali imedhibitiwa na hakuna habari za mlipuko wa virusi maalumu."
Miaka miwili iliyopita, zaidi ya mahujaji 1,300 walifariki dunia kutokana na kiharusi cha joto wakati wa ibada ya Hija kutokana na joto kali.
Mwaka huu, licha ya kushuka kwa halijoto, mahujaji 10 kutoka Indonesia, 10 kutoka Bangladesh, Wairaqi wawili na mmoja wa Malaysia wamefariki dunia kutokana na kiharusi cha joto.