Mahujaji wanasimama Arafa leo kutekeleza nguzo muhimu ya Hija
https://parstoday.ir/sw/news/world-i138640-mahujaji_wanasimama_arafa_leo_kutekeleza_nguzo_muhimu_ya_hija
Mmilioni ya Mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu, Al Kaaba, leo wanasimama katika uwanja wa Arafa katika kilele cha ibada tukufu ya Hijja.
(last modified 2026-05-26T03:32:10+00:00 )
May 26, 2026 03:17 UTC
  • Jabalur Rahma, Arafat
    Jabalur Rahma, Arafat

Mmilioni ya Mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu, Al Kaaba, leo wanasimama katika uwanja wa Arafa katika kilele cha ibada tukufu ya Hijja.

Wageni hao wa Mwenyezi Mungu, al Rahman, jana jioni walialala kwenye mahema huko Mina, na leo Jumanne watashinda kwenye Mlima Arafat wakiomba dua na kunong'ona na Mola wao Muumba.

Arafa ni jina la jangwa kubwa linalopakana na mlima Jabalur Rahma ulioko kusini mashariki mwa Makka. Tangu adhuhuri ya leo Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu, al Kaaba, wamesimama katika uwanja wa Arafa na hadithi nyingi za Kiislamu zimetaja fadhila na utukufu mkubwa wa kisimamo hicho.

Hadithi za Mtume Muhammad (SAW) na Ahlibaiti zake watoharifu zinasema kuwa Mwenyezi Mungu SW ameifanya ardhi ya Arafa ambayo ilikuwa medani ya matukio mengi muhimu ya kihistoria, kuwa mahali pa kuwapokea wageni wake wanaokwenda Hija na ameweka meza na karamu yake pembeni ya Jabalur Rahma.

Magharibi ya siku hii ya leo Mahujaji wataondoka uwanja wa Arafa na kuelekea Mash'arul Haram huko Mina na kujitayarisha kwa ajili na amali nyingine za Hijja, kama kulala Muzdalifa na kufanya amali ya Jamarat (kumpiga shetani kwa mawe saba) kesho Jumatano.

Waislamu wanaokadiriwa kuwa karibu milioni 2 wamekusanyika katika mji mtakatifu wa Makka nchini Saudi Arabia kwa ajili ya Hija ya mwaka huu.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, ambaye aliuawa shahidi katika uvamizi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran, kkatika jumbe zake kihistoria kwa Kongamano la kila mwaka la Hija, alisema Hija ilikusudiwa kuimarisha umoja miongoni mwa mataifa ya Kiislamu katika kukabiliana na ukafiri, ukandamizaji, ubeberu na masanamu watu na wasio watu.

Ayatullah Khamenei alikuwa akitoa wito kwa Umma wa Kiislamu kudumisha roho ya Hija kwa kusimama kidete bega kwa bega na Wapalestina katika mapambano yao ya kupigania uhuru.

Shahidi Imam Khamenei alikuwa akisisitiza kwamba Hija inaweza kubatilisha mipango yote ya mataifa ya kibeberu na Uzayuni inayofanywa kwa ajili ya kuharibu maadili ya wanadamu.