Niger yasimamisha vyombo tisa vya habari vya Ufaransa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i138278-niger_yasimamisha_vyombo_tisa_vya_habari_vya_ufaransa
Serikali ya Niger imetangaza kusimamisha shughuli za vyombo tisa vya habari vya Ufaransa siku ya Ijumaa, ikieleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa kutokana na “usambazaji wa mara kwa mara wa maudhui yanayoweza kuhatarisha kwa kiasi kikubwa utulivu wa umma, umoja wa taifa, mshikamano wa kijamii, na uthabiti wa taasisi za Jamhuri.”
(last modified 2026-05-10T09:30:26+00:00 )
May 10, 2026 09:28 UTC
  • Niger yasimamisha vyombo tisa vya habari vya Ufaransa

Serikali ya Niger imetangaza kusimamisha shughuli za vyombo tisa vya habari vya Ufaransa siku ya Ijumaa, ikieleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa kutokana na “usambazaji wa mara kwa mara wa maudhui yanayoweza kuhatarisha kwa kiasi kikubwa utulivu wa umma, umoja wa taifa, mshikamano wa kijamii, na uthabiti wa taasisi za Jamhuri.”

Vyombo vilivyosimamishwa ni pamoja na France 24, RFI, France Afrique Media, LSI Africa, AFP, TV5 Monde, TF1 Info, Jeune Afrique na Mediapart.

Kulingana na taarifa iliyotolewa kupitia televisheni na Taasisi ya Kitaifa ya Uangalizi wa Mawasiliano (ONC), uamuzi huo umeanza kutekelezwa mara moja, na unahusu pia “matangazo ya satelaiti, mitandao ya kebo, majukwaa ya kidijitali, tovuti na aplikesheni za simu.”

Jeshi la Niger lilichukua madaraka mwezi Julai 2023 baada ya kumpindua rais kibaraka wa Ufaransa, Mohamed Bazoum, ambaye baadaye aliwekwa kizuizini.

Hatua dhidi ya vyombo vya habari vya Ufaransa na vile vya kigeni inakuja wakati serikali ya kijeshi ya Niger imepunguza kwa kiasi kikubwa uhusiano wake na nguvu ya zamani ya kikoloni, Ufaransa, na kujitenga na washirika wa Magharibi.

Mwishoni mwa mwaka 2023, Niger iliitaka Paris kuondoa maelfu ya wanajeshi wake waliokuwa wakishiriki operesheni dhidi ya makundi yenye silaha yanayofanya shughuli nchini Niger pamoja na nchi jirani za Mali na Burkina Faso.

Tangu wakati huo, mataifa matatu yameanzisha Muungano wa Nchi za Sahel kwa ajili ya ushirikiano mpya wa ulinzi na nchi nyingine, hasa Russia.

Serikali za nchi hizo tatu zimekuwa zikishutumu mara kwa mara Ufaransa kwa kuendeleza ukoloni mamboleo, zikisisitiza azma yao ya kuimarisha “uhuru wa kitaifa.”

Vyombo vya habari vya Ufaransa na vya kigeni pia vimewahi kusimamishwa au kupigwa marufuku na serikali za Mali na Burkina Faso.

Mwaka 2024, viongozi katika mji mkuu wa Niger, Niamey, waliimarisha sheria inayofanya kosa la jinai kusambaza kidijitali “taarifa zinazoweza kuvuruga utulivu wa umma.”