Kamanda wa IRGC: Iran iko tayari kushambulia ngome za Marekani
-
Brigedia Jenerali Seyyed Majid Mousavi
Kamanda wa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (IRGC) amesema makombora ya kisasa pamoja na droni za kivita za Iran tayari zimeelekezwa dhidi ya ngome za Marekani katika eneo la Ghuba ya Uajemi, huku vikosi vikisubiri amri ya mwisho ya kushambulia.
Brigedia Jenerali Seyyed Majid Mousavi amesema katika taarifa iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii Jumamosi jioni kwamba: “Makombora na droni za anga za juu zimeelekezwa kwa adui na sasa tunasubiri amri ya kufyatua.”
Kauli ya kamanda huyo mwandamizi wa IRGC imekuja wakati mvutano kati ya Iran na Marekani ukiendelea kuongezeka katika eneo la Ghuba ya Uajemi, huku Iran ikitoa onyo kali kwamba haitavumilia uchokozi zaidi wa Marekani.
Onyo hilo limefuatia operesheni ya kulipiza kisasi za majeshi ya Iran dhidi ya uchokozi wa kijeshi za Marekani. Baada ya vikosi vya Marekani kushambulia meli za mizigo na meli za mafuta za Iran karibu na Jask, Jeshi la Wanamaji la IRGC lilijibu kwa operesheni ya haraka na yenye nguvu kwa kutumia makombora ya balistiki ya kupambana na meli, makombora ya cruise na droni zenye milipuko mikubwa.
Iran imesema mashambulizi hayo yalisababisha hasara kubwa kwa adui na kuzilazimisha meli za Marekani kuondoka eneo hilo katika hali ya taharuki.
Maafisa wa Iran wamezitaja harakati hizo za Marekani kuwa tishio kubwa kwa usalama wa usafiri wa majini katika ukanda huo pamoja na usalama wa njia za kimataifa za meli.
Jeshi la Wanamaji la IRGC nalo limesisitiza kuwa njia pekee salama na zilizoidhinishwa kwa meli kupita katika Mlango Mkakati wa Hormuz ni zile zilizowekwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Aidha limeonya kuwa hatua yoyote ya uhasama au ukiukaji kutoka kwa vikosi vya kigeni itakabiliwa na jibu la haraka, kali na la moja kwa moja.
Jeshi la Wanamaji la IRGC limesema lina udhibiti kamili wa njia hiyo muhimu ya baharini huku likisisitiza dhamira yake ya kulinda meli za Iran na kuhakikisha usalama wa Ghuba ya Uajemi.
IRGC imesema vikosi vyake vinaendelea kuwa katika hali ya tahadhari ya juu na viko tayari kujibu kwa muda wowote ili kulinda maslahi ya Iran pamoja na usalama wa eneo hilo.