Uhispania yaomboleza huku idadi ya vifo vya mafuriko ikipindukia 150
Watuu wasiopungua 158 wamefariki dunia katika maafa makubwa zaidi ya mafuriko nchini Uhispania huku waokoaji wakiendelea na shughuli ya kutafuta manusura.
Zaidi ya wafanyakazi 1,200, wakisaidiwa na ndege zisizo na rubani, wametumwa kufanya kazi ya uokoaji huku mvua ikiendelea kusababisha tisho la maafa zaidi maeneo mbali mbali ya nchi hiyo.
"Kwa sasa jambo la muhimu zaidi ni kuokoa maisha ya watu wengi iwezekanavyo," Waziri Mkuu Pedro Sánchez aliwaambia waathiriwa katika ziara ya kutembelea jamii zilizoathirika.
Lakini katika baadhi ya miji iliyoathiriwa zaidi na mafuriko ya Jumanne usiku, watu walikumbwa na kazi ya kuopoa miili kutoka kwenye matope na vifusi vya majengo yaliyoporomoka kufuatia mafuriko.
Vifo visivyopungua 155 vilirekodiwa katika mji wa Valencia, huku vingine viwili vikirekodiwa katika eneo la Castilla-La Mancha magharibi mwa jimbo hilo, na raia Muingereza, alitangazwa kufariki Andalusia.
Wakati shughuli ya kusafisha miji ikiendelea Meya wa mji mdogo wa Valencia huko Uhispania ametoa wito wa kuungwa mkono zaidi kwa raia wake.