Iran; Mwenyeji wa idadi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika Kongamano la Baraza la Wakimbizi Duniani huko Geneva Uswisi kwamba: 'Nataraji kuwa Umoja wa Mataifa na Kamisheni Kuu ya Wakimbizi Duniani zitatekeleza majukumu yao kuhusu wakimbzi na hasa kuhusu raia wa Kiafghani milioni tano wanaoishi Iran.'
Hossein Amir Abdollahian alisema Jumatano wiki hii katika Kongamano la Baraza la Wakimbizi Duniani mjini Geneva kwamba, uingiliaji mkubwa wa kijeshi na wa aina nyingine unaofanywa na madola ajinabi katika eneo letu umesababisha hali ya mchafukoge na ukosefu wa amani na hivyo kuibua wimbi la wakimbizi katika eneo zima la Asia Magharibi. Amesema, Iran imebebeshwa mzigo kutokana na sera za kutowajibika na uingiliaji kijeshi wa Marekani na waitifaki wake karibu na Iran katika kanda hii." Kongamano la Pili la Baraza la Wakimbizi Duniani lilianza Jumatano wiki hii na litaendelea hadi Alhamisi kwa kuhudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi wanachama; mwenyeji ikiwa ni serikali ya Uswisi na Kamisheni Kuu ya Wakimbizi Duniani UNHCR. Mwaka 2018 baada ya miaka kadhaa ya mazungumzo, uliratibiwa mkataba wa Kimataifa Kuhusu Wakimbizi na kupasishwa na Umoja wa Mataifa.
Kwa mujibu wa hati hiyo, ilipangwa kuwa kila mwaka kuwe kunafanyika kongamano LA kimataifa ili kujadili masuala ya wakimbizi duniani. Uingiliaji kijeshi wa nchi ajinabi, mapigano ya ndani, majanga ya kimaumbile na matatizo ya kiuchumi na haki za binadamu ni kati ya sababu kuu zinazopelekea kushuhudiwa wimbi la kuhajiri watu kwa lazima; na kwa msingi huo eneo la Asia Magharibi ni miongoni mwa maeneo yanakotoka wahajiri wengi wanaotafuta hifadhi.
Wakati huo huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa zaidi ya miongo minne sasa imekuwa ikiwapokea raia wengi kutoka nchi jirani yaani Afghanistan; ambapo idadi kubwa ya watu kutoka nchi hiyo wamelazimika kuhama makazi yao na kupewa hifadhi katika Iran ya Kiislamu kutokana na machafuko na ukosefu wa amani wa miaka kadhaa nchini kwao, vita na kukaliwa kwa mabavu nchi hiyo. Kuhusiana na suala hili, Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef) limetangaza kuwa kabla ya mwezi Agosti mwaka 2021 kulikuwa na wakimbizi milioni mbili hadi tatu wa Afghanistan nchini Iran, hata hivyo baada ya matukio ya mwaka 2021 na kuingia madarakani kundi la Taliban huko Afghanistan, wakimbizi wapya wa Kiafghani kati ya laki tano hadi milioni moja na nusu wamewasili Iran.
Ahmad Vahedi Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema mwezi Julai mwaka huu kwamba: "Makadirio yaliyofanywa kuhusu idadi ya wakimbizi wa Kiafghani waliopo nchini Iran ni zaidi ya milioni 5. "Ni wazi kuwa Iran ikiwa nchi jirani na Afghanistan na yenye mpaka mrefu na nchi hiyo inazingatia na kutoa kipaumbele maalumu kwa matukio ya Afghanistan. Aidha Iran inachukulia amani na uthabiti wa nchi hiyo ya Kiislamu kuwa sawa na amani na utulivu katika ardhi yake kinyume na baadhi ya pande za kikanda na kimataifa. Wakimbizi wa Kiafghani pia ambao wana uhusiano wa kiutamaduni, kihistoria na kidini na wananchi wa Iran hadi sasa wameweza kustafidi na suhula na huduma zote zinazotolewa na serikali ya Iran sawa kabisa na wananchi wa Iran. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amesema Iran imewaandalia wakimbizi wa Kiafghani mazingira mazuri ya kuishi kwa kuzingatia mafundisho ya Kiislamu; huku watoto wote wa Kiafghani wakiwa na uwezo wa kuandikishwa kwa ajili ya kupata elimu katika shule za Iran.
Hii ni katika hali ambayo, pamoja na uchache wa vyanzo vya kifedha na matatizo ya kiuchumi ambayo ni natija ya vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Iran, lakini kiwango cha misaada ya kimataifa kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi wa Kiafghani hapa nchini ni kidogo sasa. Ofisi ya Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia wakimbizi nchini Iran pia iliwahi kuthibitisha jambo hili na kusisitiza kuwa misaada mingi inatolewa na serikali na wananchi wa Iran na kwamba suala la kupungua misaada ya mashirika na taasisi za kimataifa kwa ajili ya kutatua matatizo ya wakimbizi hao linapasa kuhamishiwa kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ili maamuzi ya lazima yachukuliwe katika uwanja huo.
Ndio maana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikakubali kutekeleza majukumu yake sambamba na kuzitaka taasisi za kimataifa kama Umoja wa Mataifa na Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya umoja huo kutafuta ufumbuzi wa matatizo na kuwagharamia wakimbizi wanaoishi nchini Iran. Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia aliuliza swali hili muhimu na la msingi katika Kongamano la Baraza la Wakimbizi Duniani huko Geneva kwamba: 'Je, kwa nini ni nchi kadhaa tu ndizo zinabebeshwa jukumula la kuwapokea wakimbizi wengi?' Amesema: "Nchi moja haiwezi peke yake kuhudumia mzogo mkubwa wa wakimbizi duniani, ni huu si uadilifu'. Gharama za kuwatunza wakimbizi zinapasa kugawanywa kwa uadilifu kati ya nchi mbalimbali duniani."