Kuuawa shahidi, zawadi ya juhudi kubwa alizofanya Sayyid Razi katika umri wake
Mazishi ya mwili wa Sayyid Razi Mousavi yalifanyika jana Alhamisi mjini Tehran ambapo umati mkubwa wa wananchi na viongozi wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walihudhuria.
Brigedia Jenerali Razi Mousavi, mmoja wa makamanda wenye uzoefu mkubwa na wa miaka mingi katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Sepah, aliuawa shahidi Jumatatu tarehe 25 Disemba katika shambulio la kigaidi lililofanywa na utawala haramu wa Israel katika eneo la Zainabiyya katika moja ya viunga vya Damascus, mji mkuu wa Syria.
Alikuwa mmoja wa washauri wa zamani wa Kikosi cha Quds cha Sepah huko Syria na rafiki wa karibu sana wa Jenerali Qasem Soleimani, kamanda wa zamani wa Jeshi la Quds la Sepah, ambaye amekuwa akifanya kazi kwa miaka mingi katika uwanja wa kusaidia mhimili wa mapambano ya Kiislamu nchini Syria.
Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Maudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, jana asubuhi alisoma Fatiha na kuuswalia mwili wa Shahid Sayyid Razi Mousavi. Akizungumza mbele ya familia ya Shahidi Mousavi, Ayatullah Khamanei alisema: 'Kuuawa shahidi Sayyid Razi Mousavi ni zawadi aliyopata kutokana na juhudi kubwa alizofanya katika umri wake, na kumwomba Mwenyezi Mungu amjalie daraja za juu peponi.'
Shahidi Mousavi, mmoja wa maveterani wa mhimili wa muqawama, amekuwa na jukumu muhimu katika uwanja huo kwa karibu miaka 25, na kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Hossein Pulark, mkuu wa kitengo cha usaidizi cha mhimili huo, baada ya kuawa shahidi Haj Qasim Soleimani, alisikitika sana kuachwa nyuma na akitamani daima kuuawa shahidi katika mwaka wa kumbukumbu ya kuuawa shahidi Haj Qassem, na sasa maombi yake hayo yametimia na kujibiwa. Shahidi Luteni Jenerali Haj Qassem Soleimani aliuawa shahidi akiwa pamoja na Abu Mahdi al- Muhandis Naibu Mkuu wa Harakati ya Hashd Shaabi ya Iraq katika shambulio la kigaidi lililofanywa na Marekani karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Baghdad.
Mauaji ya makamanda wawili hao wa muqawama ni moja ya mipango mikuu ambayo utawala wa Kizayuni na Marekani zimekuwa zikiipanga katika miaka ya karibuni. Mauaji ya kigaidi dhidi ya Sayyid Razi na Haj Qasim Soleimani ni moja ya mifano ya wazi ya vitendo hivyo vya kihalifu, ambayo yanaonyesha wazi kukasirishwa pande hizo za maadui na kushindwa kwao mfululizo katika eneo hili la Asia Magharibi, na pia kuongezeka nguvu na uwezo wa mhimili wa muqawama.
Kwa kutambua vyema nafasi ya Shahidi Sayyid Razi katika uwanja wa kuunga mkono mhimili wa muqawama, utawala wa kigaidi wa Israel umekuwa ukipanga kwa miaka mingi njama ya kumuua shahidi huyo na huko nyuma ulitekeleza mara kadhaa mpago wa kumuua lakini bila mafamikio. Lakini sasa, baada ya operesheni yenye mafanikio na isiyo na kifani ya Kimbunga cha Al-Aqsa na kufedheheshwa kijeshi na kiintelijensia utawala wa Kizayuni na wanamapambano wa Hamas, licha ya kutumia fedha nyingi kwa madai ya kulinda usalama wake, katika kipindi cha miezi 3 iliyopita, magaidi hao wa Kizayuni kwa mara nyingine tena wametekeleza mpango wa kumuua afisa huyo wa ngazi za juu wa Sepah ili kujaribu kufidia aibu ya kushindwa kwao na Hamas katika medani ya vita na kulipiza kisasi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ni dhahiri kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupitia uwezo wake wa kisiasa, kijeshi na kimaanawi, imekuwa na nafasi muhimu katika kufelisha njama za Wazayuni na Marekani pamoja na magaidi wakiwemo wa Daesh katika eneo kwa kuimarisha nguvu ya muqawama katika eneo. Ni kutokana na ukweli huo ndipo utawala unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu na muungaji mkono wake mkuu, Marekani, daima zikawa zinapanga njama za kuwaondoa makamanda na washauri wa kijeshi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika kambi ya muqawama.
Pamoja na hayo utawala wa kigaidi wa Israel na muungaji mkono wake mkuu Marekani zinapasa kutambua kwamba mauaji ya kipofu na ya kiwoga dhidi ya makamanda kama Shahidi Razi sio tu hayatapunguza azama na nguvu ya muqawama, bali yatauimarisha zaidi na kuufanya usimame imara katika njia yake tukufu ya kupigania haki na uadilifu. Sawa kabisa kama ambavyo mauaji ya kigaidi yaliyofanywa na Marekani dhidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani hayakusimamisha mapambano bali makamanda wengine wameendeleza njia yake na mashambulio zaidi kufanywa na wanapambano dhidi ya vituo vya kijeshi vya Marekani katika eneo na muqawama kuimarika zaidi katika nchi za Palestina, Syria, Lebanon na Yemen.
Kuhusiana na suala hilo, Rais Ebrahim Risi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika ujumbe wake kwa mnasaba wa kuuawa shahidi Brigedia Jenerali Razi Mousavi amesema: “Hatua hii bila shaka ni ishara nyingine ya utawala ghasibu wa Israel kukata tamaa, kuchanganyikiwa na kutokuwa na uwezo katika eneo, na bila shaka utalipa gharama ya jinai hii."