Bwabwaja za Wazayuni dhidi ya Iran, katikati ya mgogoro
Naftali Bennett, Waziri Mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni amedai katika makala iliyochapishwa tarehe 28 Disemba (7 Januari) katika gazeti la Wall Street Journal kwamba utawala huo na Marekani zinapasa kuweka lengo la wazi la kuuangusha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Naftali Bennet pia amesema kwamba wakati wa utawala wake aliviamuru vikosi vya usalama vya Israeli viilazimishe Tehran ilipe gharama kutokana na uungaji mkono wake kwa wanamgambo wanaopigana dhidi ya Israel, na kwamba muda wa kinga ya kuadhibiwa Iran ulikuwa umemalizika.
Anaashiria operesheni iliyotekelezwa na utawala wa Kizayuni katika kituo cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH karibu na mji wa Kermanshah magharibi mwa Iran ambapo Hassan Sayyad Khodei mmoja wa askari wa Kikosi cha Quds aliuawa shahidi.
Makala hiyo ya Bennett katika Jarida la Wall Street Journal imekabiliwa na ukosoaji mkali katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) ambapo baadhi ya wakosoaji wanasema afisa huyo mkuu wa zamani wa Kizayuni amefichua masuala ya siri za juu za kijasusi za utawala wa Kizayuni bila kupata idhini ya Idara ya Udhibiti wa Kijeshi. Yakov Kats, mhariri wa zamani wa Jerusalem Post, ameandika kuhusu suala hilo kwamba: 'Niliuliza Udhibiti wa Kijeshi leo (Jumamosi) iwapo makala ya Naftali Bennett iliidhinishwa na idara hiyo au la, ikajibu: Hapana'!
Hata hivyo ni muhimu kuashiria hapa nukta chache kuhusu maropoko na madai ya waziri mkuu huyo wa zamani wa utawala wa Kizayuni. Kwanza, ni kuwa nadai hayo ni dalili nyingine inayothibitisha kuwa utawala haramu wa Israel umekuwa ukiendesha vitendo vya kigaidi dhidi ya maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kukiri huko kwa utawala wa Kizayuni katika kuhusika na operesheni za kigaidi dhidi ya Iran si tu kwamba kumefichua sura halisi ya utawala huo duniani, bali pia kunaipa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haki ya kujilinda na kujitetea na wakati huo huo kuiruhusu kuchukua hatua za kukabiliana na vitendo hivyo vya kigaidi.
Nukta nyingine ni kwamba, tajriba ya miaka ya baada ya Mapinduzi ya Kiislamu inaonyesha kuwa, maadui ukiwemo utawala wa Kizayuni na Marekani daima wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali kuzuia kufikiwa malengo matukufu ya mapinduzi hayo, ikiwa ni pamoja na kuua kigaidi makamanda wa kijeshi, wanasayansi wa nyuklia, hujuma katika viwanda na vituo vya ulinzi na kutoa mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi ili kuidhoofisha Iran. Pamoja na hayo yote lakini maadui hao daima wamekuwa wakifeli kwa sababu si tu kwamba hakujakuwa na mabadiliko ya aina yoyote katika malengo na itikadi za Jamhuri ya Kiislamu, bali ushawishi wa kimaanawi wa Iran umeongezeka katika eneo la Asia Magharibi na mfano wa wazi unaothibitisha hilo ni kuongezeka muqawama na mapambano ya Kiislamu katika eneo.
Wakati huo huo taasisi za upelelezi na usalama za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimekuwa zikitoa mapigo mazito kwa vibaraka, mamluki na mashirika ya kijasusi ya utawala wa Kizayuni nchini na katika eneo. Kwa mfano, vibaraka wanne wa timu ya hujuma na uharibifu inayohusiana na utawala huo, ambao walifanya vitendo vya uharibifu dhidi ya usalama wa Iran chini ya uongozi wa maafisa wa kijasusi wa Mossad, walitambuliwa na kukamatwa na vikosi vya usalama vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na baada ya kupitia mchakato wa kisheria, walinyongwa Jumamosi asubuhi.
Nukta nyingine ni kwamba, matamshi ya hivi karibuni ya Naftali Bennett yanaweza kutathminiwa kuwa ni jaribio la kuficha kushindwa kijeshi utawala wa Kizayuni na pia migogoro ya hivi sasa inayoukabili. Hii ni kwa sababu utawala wa Kizayuni unakabiliwa na mgogoro na mkwamo mkubwa usio na mfano wake kufuatia operesheni ya Oktoba 7 ambapo hata baadhi ya viongozi na wataalamu wa Kizayuni wanazungumzia kuanza mchakato wa kusambaratika utawala huo.