Daesh yatangaza imehusika ya shambulizi la kigaidi Kerman, Iran
Kundi la kigaidi la Daesh limedai kuhusika na milipuko miwili iliyoua watu 84 na kujeruhi wengine wengi katika kumbukumbu ya kamanda mkuu wa kupambana na ugaidi, Luteni Jenerali Qassem Soleimani katika mji wa Kerman, kusini mashariki mwa Iran.
Katika taarifa iliyotumwa kwenye ukurasa wake wa Telegram, kundi hilo la kigaidi limesema wanachama wawili walilipua mikanda yao ya vilipuzi katika umati wa watu waliokuwa wamekusanyika kwenye makaburi kwa ajili ya kumbukumbu ya mauaji yaliyofanywa na Marekani dhidi ya Jenerali Soleimani.
Hapo awali, chanzo ambacho hakikutajwa jina kililiambia Shirika rasmi la Habari la Iran (IRNA) kwamba mlipuko wa kwanza karibu na makaburi ya Kerman, mji alikozaliwa Jenerali Soleimani, "ulitokea baada ya mshambuliaji kujilipua na kujitoa uhai".
Chanzo hicho kimedokeza kuwa: "Mwili wa gaidi aliyejilipua katika tukio la kwanza ulikatwa vipande vipande kutokana na mlipuko huo na uchunguzi wa kumtambua unaendelea."
Chanzo hicho kimeiambia IRNA kwamba sababu ya mlipuko wa pili ilikuwa sawa na ile ya mlipuko wa kwanza."
Chanzo hicho kimesema, mahali palipotokea milipuko hiyo, ni kilomita 1.5 na kilomita 2.7 kutoka alikozikwa Jenerali Soleimani, na kwamba magaidi hao hawakuweza kupita kwenye milango ya ukaguzi katika eneo hilo.
Mapema jana Alhamisi, chombo cha juu cha usalama cha Iran kiliyapa majukumu mashirika ya ujasusi, usalama na sheria nchini kuwabaini na kuwaadhibu mara moja wale waliohusika na milipuko ya Jumatano ambayo imeua makumi ya watu huko Kerman.