Abdollahian azionya Marekani na Uingereza: Komesheni mara moja vita dhidi ya Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i107256-abdollahian_azionya_marekani_na_uingereza_komesheni_mara_moja_vita_dhidi_ya_yemen
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezionya Marekani na Uingereza na kuzitaka zisitishe mara moja vita dhidi ya Yemen.
(last modified 2024-01-15T23:48:01+00:00 )
Jan 15, 2024 23:48 UTC
  • Abdollahian azionya Marekani na Uingereza: Komesheni mara moja vita dhidi ya Yemen

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezionya Marekani na Uingereza na kuzitaka zisitishe mara moja vita dhidi ya Yemen.

Hussein Amir-Abdollahian alisema hayo jana katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran na Subrahmanyam Jaishankar, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa India na kusisitiza kwamba, na kuziambia Marekani na Uingereza kwamba, vita sio suluhisho.

Katika kikao hicho na waandishi wa habari, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono kwa dhati usalama wa meli na usafiri wa baharini katika eneo na kuzionya Marekani na Uingereza kusimamisha mara moja vita dhidi ya Yemen.

Abdollahian amesema: Iran daima imekuwa ikisisitiza juu ya kuepusha kupanuliwa wigo wa vita na kwamba, kulindwa usalama wa safari za baharini na meli ni jambo linalotiliwa mkazo na Iran na suala hilo limesisitizwa katika uhusiano wa kirafiki wa Tehran na Serikali ya Uokoaji wa Kitaifa ya Yemen.

Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran na India wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari

 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: Marekani haiwezi kusimama pamoja na Israel kwa nguvu zake zote na kushiriki katika mauaji ya maelfu ya raia katika Ukanda wa Gaza na wakati huo kuwataka wengine kuwa watulivu na wenye  kujizuia.

Amir Abdollahian ameongeza kuwa, Benyamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel anakabiliwa na kesi mbalimbali katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na historia yake imefikia tamati, huku Ikulu ya Marekani ikifungamanisha maslahi ya wananchi wa Marekani na utawala huo wa kibaguzi.