Marekani yatiwa kiwewe na shambulio la IRGC dhidi ya kituo cha Mossad
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i107296-marekani_yatiwa_kiwewe_na_shambulio_la_irgc_dhidi_ya_kituo_cha_mossad
Maafisa wa Marekani wameghadhabishwa mno na hatua ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) kufanya shambulio la makombora dhidi ya kituo kikuu cha ujasusi cha shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel Mossad katika eneo la Kurdistan ya Iraq.
(last modified 2024-01-16T23:08:30+00:00 )
Jan 16, 2024 23:08 UTC
  • Marekani yatiwa kiwewe na shambulio la IRGC dhidi ya kituo cha Mossad

Maafisa wa Marekani wameghadhabishwa mno na hatua ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) kufanya shambulio la makombora dhidi ya kituo kikuu cha ujasusi cha shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel Mossad katika eneo la Kurdistan ya Iraq.

Balozi wa Marekani nchini Iraq, Alina Romanowski ametumia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X (Twitter) kueleza hamaki zake kufuatia shambulio hilo la SEPAH la ulipizaji kisasi.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Marekani amenukuliwa na kanali ya televisheni ya Tigris akidai kuwa, eti shambulio hilo la SEPAH limelenga raia. 

Hii ni katika hali ambayo, IRGC imetangaza kuwa, shambulio lake la makombora katika eneo la Kurdistan ya Iraq limelenga na kukiangamiza kikamilifu kituo cha kijasusi cha Mossad katika eneo hilo.

Balozi wa Marekani nchini Iraq, Alina Romanowski ameendelea kubwabwaja kwa kudai kuwa, shambulio hilo la IRGC, ambalo ni la ulipizaji kisasi na ambalo linaendana na sheria za kimataifa kuhusu kujihami unapochokozwa au kushambuliwa, eti limekanyaga mamlaka ya kujitawala Iraq.  

Balozi wa Marekani nchini Iraq, Alina Romanowski

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limefafanua kuwa, kituo hicho cha Mossad kilitumika "kuendeleza operesheni za kijasusi na kupanga vitendo vya kigaidi" katika eneo zima, hususan nchini Iran.

Katika taarifa yake hiyo, SEPAH imesema shambulio hilo ni ishara ya uwezo kamili na wa hali ya juu wa kiintelijensia lililonao Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa vituo na shughuli unazoendesha utawala wa Kizayuni katika eneo.

IRGC imesisitiza kuwa, shambulio hilo la makombora dhidi ya kituo cha Mossad ni la kulipiza kisasi cha mauaji ya hivi karibuni ya kigaidi ya makamanda wa vikosi vya Muqawama hasa wa jeshi hilo yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni.