Raisi awahimiza Waislamu kushikamana na mafundisho ya Uislamu na kukabiliana na Israel
Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa lau nchi zote za Kiislamu zingeongozwa na Qur’ani na kuwa adui wa madhalimu, utawala wa Kizayuni wa Israel usingethubutu kuwaua kwa umati Wapalestina huko Ukanda wa Gaza.
Sayyid Raisi aliyasema haya jana katika hafla ya kufunga Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani mjini Tehran.
Amesema kuwa Qur'ani ni kitabu chenye mwongozo kwa wanaadamu wote, ijapokuwa baadhi ya watu hawapendi kuongoka. Amesisitiza ulazima wa kufanyika juhudi za kukuza ufahamu, usomaji na ujuzi wa Qur'ani na akasema: Leo hii wajibu wa mahafadh wote, wasomaji na wenye kuifahamu vyema Qur'ani ni kueneza maarifa ya dini, na kuelimisha Umma na jamii kwa kutumia Aya zenye nuru za Qur'ani Tukufu.
Dakta Raisi amesisitiza kwamba leo hii huko Gaza "utukufu" wote umesimama kukabiliana "maovu" yote na kuongeza kuwa: Dulma tunayoishuhudia leo dhidi ya wanadamu ni matokeo ya kuacha kutekelezwa mafundishi ya Qur'ani Tukufu. Amesema, njia ya kusahihisha hali hiyo ni kurejea katika Qur'ani, kuunda Umma wa Kiislamu unaoshikamana na Qur'ani, Mtume Muhammad (SAW) na Ahlul-Bayt na kufuata Aya na maagizo ya Qur'ani Tukufu.
Rais Ebrahim Raisi amesema kuwa Marekani ni mhimili wa shari katika dunia ya leo na kwamba lau Waislamu wangeongozwa na kitabu chao kitakatifu na mafundisho ya Mtume Muhammad (SAW), nchi hiyo isingeweza kuyapigia kura ya veto maazimio ya Umoja wa Mataifa ya kutaka kusitishwa vita katika Ukanda wa Gaza.
Juzi Jumanne Marekani, kwa mara nyingine tena, iliukingia kifua utawala wa Israel katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa hatua yake ya kulipiga veto azimio la UN lililokuwa limeandaliwa na Algeria. Azimio hilo lilitaka kusitishwa vita kwa sababu za kibinadamu Ukanda wa Gaza haraka iwezekanavyo. Hadi sasa Wapalestina zaidi ya 29,000 wameuliwa shahidi katika mashambulizi ya Israel tangu Oktoba 7 mwaka jana.
Mwishoni mwa hotuba yake ya kuhitimisha Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu mjini Tehran, Rais wa Iran amesema: Tunanyoosha mikono ya udugu na mshikamano kwa Waislamu wote duniani na tunaamini kuwa Qur'ani inaweza kuwa mhimili wa umoja na maisha ya amani kwa Waislamu na wafuasi wote wa dini, kaumu na lugha tofauti.