Raisi: Wote ni washindi katika uchaguzi wa Iran kwani wametekeleza wajibu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i109010-raisi_wote_ni_washindi_katika_uchaguzi_wa_iran_kwani_wametekeleza_wajibu
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa uchaguzi katika Jamhuri ya Kiislamu hauna walioshindwa na kwamba hakuna tofauti yoyote kuhusu nani atashinda.
(last modified 2024-03-01T06:41:11+00:00 )
Mar 01, 2024 06:41 UTC
  • Raisi: Wote ni washindi katika uchaguzi wa Iran kwani wametekeleza wajibu

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa uchaguzi katika Jamhuri ya Kiislamu hauna walioshindwa na kwamba hakuna tofauti yoyote kuhusu nani atashinda.

Rais Ebrahim Raisi ameyasema hayo baada ya kupiga kura yake kwenye sanduku la kura kwa ajili ya uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiisalmu (Bunge) na Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu mapema leo Ijumaa.

Katika mahojiano na waandishi habari, Rais Raisi amesema katika mahojiano kuwa washindi wa uchaguzi uliowasilishwa ni wapiga kura na wagombea kwani wametimiza wajibu wao.

Akiutaja uchaguzi wa leo kuwa ni mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu, Rais wa Iran amebainisha kuwa, makundi mbalimbali ya Iran yanaundwa kupitia kura za wananchi.

Rais Raisi ameutaja uchaguzi huo kuwa ni sikukuu ya kweli ya taifa kubwa la Iran na akasema, "Uchaguzi ni alama ya mshikamano na umoja wa kitaifa; leo makundi, mirengo yote ya kisiasa imejitokeza jukwaani kwa kuwatambulisha wagombea wao kwa wananchi wetu, ili siku hii iwe tukufu kwa taifa la Iran."

Rais Ebrahim Raisi akipiga kura

Uchaguzi wa duru ya 12 ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) na Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu umefanyika leo Ijumaa kote nchini ambapo wagombea wanawania viti 290 vya Bunge na 88 vya Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa nchi.

Kampeni za uchaguzi huo ambazo zilianza wiki moja iliyopita zilimazika asubuhi ya jana kwa mujibu wa kifungu cha Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Zaidi ya wagombea 15,200 wanawania viti 290 vya ubunge, 30 kati ya hivyo ni vya mji mkuu, Tehran, ambao unatambuliwa kuwa jimbo kubwa zaidi la uchaguzi nchini. Wabunge hao huhudumu kwa kipindi cha miaka minne.

Wapiga kura wa Iran, ambao idadi yao ni milioni 61, 172 elfu na 298, pia watachagua wajumbe wa Baraza la Wataalamu, linalojumuisha wanachama 88 wanaohudumu kwa kipindi cha miaka 8.

Wanawake Iran wakipiga kura kwa mfumo wa kielektroniki ambao unatumika katika baadhi ya vituo vya kupigia kura

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran inaonesha kuwa, idadi ya watu waliojiandikisha kugombea viti vya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) imevunja rekodi ya ile iyosajiliwa tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, mwaka 1979.

Taarifa hiyo inasema, wagombea 15,200 wameidhinishwa na vyombo husika kuwania viti vya Bunge, idadi ambayo inaweka rekodi mpya tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979.

Aidha orodha ya wagombea waliotimiza masharti inajumuisha majina ya wanawake 1,713, ambayo ni zaidi ya mara mbili ya 819 waliogombe viti vya Bunge hapa nchini mwaka 2020.