Zoezi la kuhesabu kura Iran linaendelea; matokeo yaanza kutangazwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i109038-zoezi_la_kuhesabu_kura_iran_linaendelea_matokeo_yaanza_kutangazwa
Zoezi la kuhesabu kura za uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) na Baraza la Watalaamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran linaendelea.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Mar 02, 2024 04:04 UTC
  • Zoezi la kuhesabu kura Iran linaendelea; matokeo yaanza kutangazwa

Zoezi la kuhesabu kura za uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) na Baraza la Watalaamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran linaendelea.

Mchakato wa kuhesabu kura ulianza mara tu baada ya kumalizika zoezi la upigaji kura. Baadhi ya majimbo ya uchaguzi wa Iran uliofanyika jana matokeo yake yameanza kutangazwa.

Kwa mujibu wa ripoti, zaidi ya waandishi 350 kutoka vyombo vya habari 160 na nchi 20 waliripoti uchaguzi wa jana wa duru ya 12 ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) na Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Uchaguzi wa duru ya 12 ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) na Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ulifanyika jana Ijumaa kote nchini ambapo wagombea wanawania viti 290 vya Bunge na 88 vya Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa nchi.

Zaidi ya wagombea 15,200 wanawania viti 290 vya ubunge, 30 kati ya hivyo ni vya mji mkuu, Tehran, ambao unatambuliwa kuwa jimbo kubwa zaidi la uchaguzi nchini. Wabunge hao huhudumu kwa kipindi cha miaka minne.

 

Wapiga kura wa Iran, ambao idadi yao ni milioni 61, 172 elfu na 298, pia walipiga  kura kuwachagua wajumbe wa Baraza la Wataalamu, linalojumuisha wanachama 88 wanaohudumu kwa kipindi cha miaka 8. Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iran inaonesha kuwa, idadi ya watu waliojiandikisha kugombea viti vya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) imevunja rekodi ya ile iyosajiliwa tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, mwaka 1979.