SEPAH: Kimbunga cha al Aqsa kimethibitisha kuwa kambi ya muqawama imeshikamana vilivyo
Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amesema: Operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa imethibitisha kwamba safu ya kambi ya muqawama imeshikamana barabara na ina uwezo mkubwa, ingawa bado haijatumia uwezo wake wote, na pia imethibitisha kwamba hakuna mtu anayeweza kupuuza nguvu za kambi hiyo.
Kamanda Qaani, amebainisha pia kuwa kuwalinda wanyonge na watu wanaodhulumiwa kuna nafasi maalumu katika utamaduni wa kidini wa Iran ambapo hivi sasa watu wanaodhulumiwa zaidi duniani ni Wapalestina.
Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa, nguzo za kambi ya muqawama zinaendelea kuwa imara siku baada ya siku kutokana na ikhlasi ya mwanzilishi wake yaani Imam Khomeini MA na kwa juhudi kubwa za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei hadi leo hii.
Ameongeza kuwa, Unapoangalia hali waliyokuwa nayo wanamapambano wa Palestina katika miongo miwili iliyopita utaona kwamba vijana wa Palestina walikuwa wakijihami kwa mawe na mikono mitupu, lakini hivi sasa wanamapambano wa Palestina hasa vikosi vya HAMAS wameendesha operesheni ya kishujaa na kimbunga ya al Aqsa, wakitegemea imani yao thabiti, ushujaa na silaha walizo nazo, na wamefanikiwa kuuweka kwenye wakati mgumu sana utawala wa Kizayuni wa Israel.
Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH vile vile amesema, utawala wa Kizayuni unatia chumvi na kukuza sana kile unachodai ni mafanikio yake kwa kutumia vyombo vyake vya habari na kuongeza kuwa, mafanikio pekee iliyopata Israel kwenye vita vya Ghaza ni kuua kikatili takriban watu elfu 40, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wadogo.