Iran: Majanga ya Gaza ni maabara ya kupima haki za binadamu
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema kuwa, majanga chungu nzima yaliyowapa watu wa Ukanda wa Gaza katika kipindi cha miezi 6 iliyopita ni maabara ya kupima ni kwa kiwango gani nchi na jamii ya kimataifa zinavyoheshimu haki za binadamu.
Nasser Kanani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, aliandika jana Ijumaa katika ujumbe wake kwenye ukurasa wa mtandao wa kijamii wa "X", kwamba majanga chungu nzima ya Gaza katika kipindi cha miezi 6 iliyopita ni maabara ya kupima ni kwa kiwango gani serikali za nchi mbalimbali, taasisi na mashirika ya kimataifa yanavyotekeleza majukumu yao ya kibinadamu, kimaadili, kisheria na kimataifa kuhusiana na haki za binadamu.
Kan'ani ameongeza kuwa, msimamo wa nchi na viongozi wa serikali zinazodai kutetea haki za binadamu kuhusiana na jinai mbaya iliyofanywa na askari wa utawala wa kibaguzi wa Israel katika pwani ya kusini magharibi mwa Gaza ya kuwaua na kuwazika vijana wawili wa Kipalestina ambao hawakuwa na silaha, unaonesha ni kwa kiasi gani wanatekeleza kauli mbiu zao na madai ya kutetea haki za binadamu.
Picha za video zilizonaswa na televisheni ya Al Jazeera ya Qatar zinaonyesha wanaume wawili wa Kipalestina wasio na silaha, mmoja akipunga hewani kipande cha kitambaa cheupe mara kwa mara kuashiria kujisalimisha, kabla ya askari katili wa jeshi la kigaidi la utawala wa Kizayuni wa Israel kuwapiga risasi na kisha kuzifukia maiti zao kwenye kifusi kwa kutumia tingatinga karibu na mji wa Gaza.
Profesa Richard Falk, Ripota Maalumu wa zamani wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu huko Palestina amesema, ufyatuaji risasi huo uliofanywa na askari wa Kizayuni ni "uthibitisho wa wazi wa kuendelezwa ukatili wa Israel huko Gaza" ambao umekuwa kama "jambo la kila siku".
Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani [CAIR] pia limetoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuchunguza video inayoonyesha wanajeshi wa utawala wa Israel wakiwapiga risasi bila sababu Wapalestina wawili wanaoonekana kuwa hawana silaha kisha kuzifukia maiti zao kwa buldoza.