May 04, 2024 06:58 UTC
  • Vyuo vikuu zaidi vya Iran vyakaribisha waliofukuzwa kwenye vyuo vya Marekani

Vyuo vikuu viwili maarufu vya Iran vimejiunga na vyuo vingine vikuu kadhaa hapa nchini na kutoa ufadhili wa masomo na mazingira bora ya kielimu kwa wanafunzi ambao wamefukuzwa kwenye vyuo vikuu vya Marekani kwa sababu tu ya kuandamana wakipinga mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel huko Gaza na misaada ya kijeshi ya Marekani kwa utawala huo.

Taarifa hiyo ilitolewa Alhamisi wiki hii na marais wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Iran (IUST) na Chuo Kikuu cha Allameh Tabataba'i (ATU).

Mansour Anbia, rais wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Iran (IUST) amesema: IUST inajitolea kuwapokea wanafunzi waliofukuzwa kwenye vyuo vikuu vya Marekani kwa sababu ya kuwaunga mkono Wapalestina na kuwatayarishia mazingira na bonasi sawa na walizokuwa wakipewa katika nchi yao." 

Rais wa Chuo Kikuu cha Allameh Tabataba'i (ATU), Abdollah Mo’tamedi pia amesema chuo hicho "kimejitayarisha kutoa ufadhili wa masomo na kufundisha lugha ya Kiajemi kwa wanafunzi na maprofesa waliofukuzwa katika vyuo vikuu vya Marekani kwa sababu tu ya kuwaunga mkono Wapalestina."

Awali, Sayyid Mahmoud Aghamiri, mkuu wa Chuo Kikuu cha Shahid Beheshti mjini Tehran, alisema chuo hicho kitatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Marekani na Ulaya, ambao wamefukuzwa kwa kushiriki maandamano ya kuunga mkono Palestina.

Mamia ya wanafunzi wa vyuo vikuu wamekamatwa Marekani kwa kupinga mauaji ya Israel huko Gaza

Jumatano iliyopita, Chuo Kikuu cha Shiraz kilikuwa kituo cha kwanza cha kitaaluma cha Iran kutoa ufadhili wa kuendelea na masomo katika chuo hicho cha kifahari kwa wanafunzi na maprofesa wa Kimarekani ambao wamefukuzwa au kutishiwa kufukuzwa.

Wanafunzi wa vyuo vikuu vya Marekani walianza maandamano yao Aprili 18, wakipinga vita na misaada ya serikali ya Washington kwa utawala katili wa Israel unaoendelea kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina. Hadi sasa Wapalestina 34,622 wameuawa, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.