May 25, 2024 12:20 UTC

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema mahuhudurio makubwa ya wananchi Waislamu wa Iran kwenye mazishi na misafara ya kuwaaga na kuwaenzi Rais Ebrahim Raisi wa Iran na mashahidi wenzake yameidhihirishia dunia kuwa, Wairani ni waaminifu na wamefungamana na nara za Mapinduzi ya Kiislamu.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo alipowatembelea jamaa za famili ya Shahidi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian hapa Tehran, ambapo amepongeza mahudhurio makubwa ya wananchi wa Iran katika mazishi na maziko ya mashahidi hao wa kuwahudumia wananchi katika miji mbali mbali ya Iran ikiwemo Tabriz, Qom, Mashhad, Maragheh, na Zanjan.

Kiongozi Muadhamu amemtaja Amir-Abdollahian kama mchapakazi asiyechoka, na kwamba jitihada zake pamoja na za Sayyid Rais hapa nchini Iran na katika uga wa kimataifa zimenakiliwa kwa kina kwenye madaftari ya kumbukumbu. 

Ayatullah Khamenei ameashiria kampeni na propaganda za maadui wanaodai kuwa wananchi wa Iran wajiweka mbali na Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza kuwa, mikusanyiko na misafara ya kuwaaga mashahidi hao wa Iran kwa mara nyingine tena imedhihirisha kushikamana kwa wananchi wa Iran na Mapinduzi na nara za Mapinduzi ya Kiislamu.

Kiongozi Muadhamu na wanafamilia ya Amir-Abdollahian na mashahidi wengine

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Jumatano iliyopita alifika nyumbani kwa Rais Sayyid Ebrahim Rais wa Iran na kumtaja shahidi huyo kuwa dhihirisho la nara za Mapinduzi ya Kiislamu. 

Mapema leo Jumamosi, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliongoza khitma na kikao cha kumbukizi na kuwaenzi mashahidi wa khidma katika Husseiyniyya ya Imam Khomeini hapa jijini Tehran.

Katika kikao hicho, Ayatullah Ali Khamenei amewapongeza na kuwaenzi mashahidi wengine wa ajali ya helikopta iliyotokea Jumapili iliyopita katika mkoa wa Azerbaijan Mashariki, kaskazini magharibi mwa Iran, akiwemo Imam wa Swala ya Ijumaa katika jiji la Tabriz, Mohammad Ali Al-e-Hashem, na Malik Rahmati, Gavana wa mkoa wa Azarbaijan Mashariki.

Kiongozi Muadhamu akiongoza khitma ya mashahidi wa khidma katika Husseiyniyya ya Imam Khomeini jijini Tehran

Mbali na maelfu ya wananchi wa Iran, lakini pia mabalozi na wawakilishi wa mataifa mbali mbali hapa nchini wamehudhuria marasimu hayo. Kadhalika Rais Abdul Latif Rashid wa Iraq ambaye aliwasili hapa Tehran mapema leo, ameshiriki kwenye marasimu hayo.

Aidha shughuli hiyo imedhuhuriwa na jamaa za familia za mashahidi, maafisa wa ngazi za juu wa ulinzi na usalama wa Iran, pamoja na wasomaji wa Qur'ani Tukufu na mashairi na tungo za kuwasifu Ahlul-Bayt (AS) kutoka ndani na nje ya nchi.

Tags