Spika wa Bunge la Iran: Ulimwengu umeanza kusikia sauti ya Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i112454-spika_wa_bunge_la_iran_ulimwengu_umeanza_kusikia_sauti_ya_palestina
Spika wa Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa, ulimwengu umeanza kusikia sauti ya Palestina.
(last modified 2024-06-01T22:58:47+00:00 )
Jun 01, 2024 22:58 UTC
  • Spika wa Bunge la Iran: Ulimwengu umeanza kusikia sauti ya Palestina

Spika wa Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa, ulimwengu umeanza kusikia sauti ya Palestina.

Muhammad Bagher Qalibaf, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hayo alipokuwa akizungumza katika mkutano wa kimataifa wa "Gaza, Madhulumu Aliyesimama Kidete" hapa mjini Tehran na kusisitiza umuhimu wa jamii ya kimataifa kuwa pamoja na Palestina.

Spika Qalibaf ameashiria kulaaniwa hivi karibuni kwa Israel na Mahakama ya Kimataifa ya Haki na kuongezeka wimbi la uungaji mkono kwa Palestina ambalo sasa limefika mpaka Ulaya kutoka Rafah.

Aidha amesema, leo hii dhamiri za watu huru wa dunia zimeamka na kuona kile kinachotokea Palestina, na tunashuhudia mikuusanyiko ya watu wengi katika miji ya Ulaya na Marekani kwa ajili ya kuwaunga mkono wananchi wanamuqawama wa Gaza na Rafah, wimbi la kulitambua Taifa huru la Palestina huku Mahakama ya Kimataifa ya The Hague ikilaani jinai za utawala haramu wa Israel.

Washiriki wa mkutano wa Gaza; Madhulumu Aliyesimama Kidete

 

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema pia kuwa, vyuo vikuu vya Ulaya na Marekani vimegeuka kuwa vyumba vya madarasa kwa ajili ya harakati za ukombozi na uhuru wa Palestina licha ya ukandamizaji unaofanywa na waungaji mkono wa utawala ghasibu na haramu wa Israel.

Kadhalika amenyesha imani na matumaini kwamba, umoja na ustahimilivu mbele ya ukandamizaji hatimaye vitaleta ushindi.