Kamanda: Nchi za kigeni zina hamu ya kununua droni za Iran
(last modified Mon, 10 Jun 2024 03:22:56 GMT )
Jun 10, 2024 03:22 UTC
  • Kamanda: Nchi za kigeni zina hamu ya kununua droni za Iran

Kamanda wa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ni moja ya madola yenye nguvu kubwa za ndege zisizo na rubani (droni) duniani.

Brigedia Jenerali Hamid Vahedi alisema hayo alipiotembelea kambi ya Kikosi cha Anga cha Jeshi la Iran katika mji wa bandari wa Bushehr, kusini mwa Iran na kueleza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imepiga hatua kubwa katika utengenezaji wa ndege za kisasa kabisa zisizo na rubani baada ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979, licha ya vikwazo vya maadui.

Kamanda Vahedi ameashiria hatua kubwa zilizopigwa na Jamhuri ya Kiislamu katika sekta ya ulinzi na upanuzi wa ushirikiano wa kijeshi  kati ya Iran, nchi za eneo hili na kimataifa na kusema: Wateja wengi wa kigeni wana hamu ya kununua droni za Iran. 

Ameeleza bayana kuwa, uuzaji nje wa zana za kijeshi za Iran umeongezeka pakubwa katika miaka ya karibuni na kuongeza kwa kusema, Tehran ina uwezo mkubwa katika uundaji wa droni na kuzikarabati. 

Brigedia Jenerali Hamid Vahedi

"Nchi nyingi sana za kigeni zimetangaza azma na hamu ya kununua ndege zisizo na rubani za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran," amesisitiza Kamanda wa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Iran.

Ikumbukwe kuwa, mwishoni mwa mwaka uliopita 2023, Reza Talaei-Nik, Naibu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Usimamizi na Mpango Mkakati ambaye pia ni Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Iran alifichukua kuwa nchi kadhaa za Ulaya zimetuma maombi yao ya kutaka kuuziwa ndege zisizo na rubani za Iran.

Tags