Jun 13, 2024 02:27 UTC
  • Iran yashtushwa na kushtadi vita vya wenyewe kwa wenyewe Sudan

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa ameshtushwa na ripoti za kuogofya kuhusu idadi kubwa ya watu waliouawa kutokana na shambulio lililolenga kijiji cha Wad al-Nura katika jimbo la al-Jazeera nchini Sudan.

Naseer Kan'ani huku akiashiria ripoti za vyombo vya habari zinazosema kuwa mamia ya watu waliuawa na kujeruhiwa katika hujuma hiyo ya umwagwaji damu huko Sudan amesema shambulizi hilo linashtua na kuogofya.

Ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kivitendo za kusimamisha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan, ambayo yamepelekea idadi kubwa ya watu wasio na hatia kuuawa au kujeruhiwa.

Vyombo vya habari viliripoti kuwa, zaidi ya watu 150 waliuawa katika kijiji cha Wad al-Nura katika mashambulizi yaliyoanza Jumatano ya wiki iliyopita, yanayodaiwa kufanywa na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF). Mapigano makali yameendelea kuripotiwa Sudan jimboni Darfur Kaskazini, hususan mjini el-Fasher na viunga vyake, kati ya Jeshi la Kitaifa la Serikali SAF na wanamgambo wa RSF. 

Mapigano ya silaha yalianza huko Sudan Aprili 15 mwaka jana kati ya jeshi la nchi hiyo (SAF) linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan ambaye ni kiongozi wa Sudan na wanamgambo wa RSF ambao kamanda wao ni Hamdan Dagalo.

Athari za mapigano ya umwagaji damu Sudan

Hadi sasa juhudi za upatanishi wa kimataifa za kuhitimisha mapigano hayo yaliyoua na kujeruhi maelfu ya watu na kuzishawishi pande hasimu kuketi kwenye meza ya mazungumzo, zimegonga mwamba.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inazipa pole familia zilizopoteza wapendwa wao kwenye mgogoro unaendelea kushtadi kila uchao Sudan, akisisitiza kuwa jamii ya kimataifa hasa mashirika ya haki za binadamu yana wajibu wa kuchukua hatua athirifu za kuhitimisha mapigano katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

 

Tags