Jun 21, 2024 10:54 UTC
  • Radiamali ya Iran kwa hatua ya kihasama ya Canada dhidi ya SEPAH

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amelaani vikali hatua ya kihasama na kiuadui ya serikali ya Canada dhidi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH).

Nasser Kanani Chafi, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran, amelaani vikali hatua ya kisiasa, isiyo ya kawaida na isiyo ya busara ya serikali ya Canada ya kulitangaza Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni la kigaidi.

Serikali ya Canada, ambayo yenyewe inahesabiwa kuwa mmoja wa waungaji mkono wakuu wa makundi ya kigaidi na ardhi ya nchi hiyo ni maficho na makazi yao, Jumatano ya juzi (19 Juni) katika hatua ya uadui na kinyume na sheria za kimataifa, ililiweka jina la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika kile kinachoitwa eti " orodha ya kigaidi.

Nasser Kanani, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran

 

Nasser Kanani, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran sambamba na kulaani hatua hiyo ya kisiasa na isiyo ya kawaida ya serikali ya Canada ya kulitangaza kuwa la kigaidi Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (SEPAH), amesema kuwa, uamuzi huu wa serikali ya Ottawa ni hatua ya kiuadui na kinyume na viwango vinavyokubalika na sheria za kimataifa, ikiwemo kutoingilia masuala ya ndani ya tawala na nchi nyingine na kuihesabu hatua hiyo kuwa ni mfano wa hujuma dhidi ya mamlaka ya kitaifa ya Iran.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ameeleza kwamba, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) ni taasisi ya kiutawala iliyotokana na muktadha wa taifa la Iran na ina utambulisho rasmi na wa kisheria unaotokana na katiba ya Jamhuri ya Kiislamu, ambayo, pamoja na vipengele vingine vya jeshi, ina jukumu la kulinda usalama wa taifa na mipaka ya Iran, pamoja na kuchangia usalama imara na utulivu katika eneo ili kukabiliana na ugaidi.

Hatua ya kihasama ya Canada dhidi ya Iran

 

Serikali ya Canada, ambayo imeendeleza siasa za uadui dhidi ya Iran katika miaka ya hivi karibuni, imekuwa hifadhi na kimbilio la mafisadi wakubwa kama vile Mahmoud Khavari (aliyekuwa Mkuu wa Benki ya Taifa ya Iran) na harakati za kigaidi na maadui wa taifa la Iran, hasa kundi la kigaidi la Munafiqeen, sasa imechukua hatua ya kipropaganda dhidi ya Jeshi la  Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH).

Baadhi ya wabunge wa Canada kwa muda mrefu wamekuwa wakitaka jeshi la SEPAH kujumuishwa katika orodha ya magaidi, lakini serikali ya kiliberali ya Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau ilijizuia kufanya hivyo na kuonya kwamba inaweza kuwa na matokeo yasiyoridhisha.

Hata hivyo, serikali ya Canada imewahi mara kadhaa kukijumuisha Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) katika orodha ya magaidi. Ukweli wa mambo ni kuwa, hii si mara ya kwanza suala la kuwekwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika orodha ya magaidi linafuatiliwa na baadhi ya nchi na shakhsia za Magharibi.

Jaribio kama hilo limefanywa mara nyingi huko nyuma. Kwa mfano, wakati yalipotokea machafuko na vurugu nchini Iran mwaka 2022, Wamagharibi waliweka katika ajenda zao suala la kuwaita Walinzi wa Mapinduzi kuwa ni magaidi. Mafanikio ya  Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya ugaidi hususan mchango wake muhimu na mashuhuri katika vita dhidi ya ugaidi wa Daesh huko Syria na Iraq ni sababu nyingine ambayo imezidisha uadui wa nchi za Magharibi dhidi yake.

Nembo ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (SEPAH)

 

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni taasisi rasmi na ya kiutawala ambayo imekuwa na nafasi muhimu katika kuhakikisha usalama wa taifa la Iran na eneo zima hususan katika mapambano dhidi ya ugaidi na isitoshe, halijaacha bila majibu mashambulizi ya utawala wa Kizayuni ambapo yote hayo yamepelekea kushadidi uadui wa madola ya Magharibi na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya asasi hii ya Kimapinduzi.

Pamoja na hayo, hatua ya kuwaita magaidi Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) katika nchi za Magharibi kabla ya kila kitu, ni kielelezo cha kushindwa kwa maadui kukabiliana na mchango wa jeshi hili na vilevile kutokuwa na uwezo wa kusimamisha mchakato wa kuimarisha nafasi ya muqawama katika mfumo wa kisiasa na kiusalama katika eneo la Asia Magharibi. Ukweli ni kwamba, tuhuma za ugaidi na vikwazo si tu kwamba, hakutazuia kusonga mbele na kupiga hatua muqawama na mihimili yake katika eneo, bali hilo litaimarisha nia na azma ya kujiendeleza zaidi.

Tags