Kamanda wa Kikosi cha Quds cha SEPAH aonana na makamanda wa muqawama
Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH ametembelea maeneo tofauti ya operesheni za kambi ya muqawama za kupambana na Wazayuni na kuonana ana kwa ana na maafisa na makamanda wa muqawama kwenye maeneo hayo.
Hayo yameripotiwa na shirika la habari la Tasnim ambalo limeongeza kuwa, Brigedia Jenerali Esmail Qaani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) ameonesha kivitendo uungaji mkono kamili wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kutembelea maeneo tofauti kunakofanyika operesheni za kuliunga mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina na kukabiliana na njama za Kizayuni duniani zinazoendeshwa na madola ya kibeberu ya Magharibi.
Kamanda Qaani ametangaza wazi kwamba, kuunga mkono mapambano na muqawama hasa wa Palestina na hususan kutotetereka wananchi wa Ghaza, ni katika siasa za kimkakati na za daima za Iran. Nguzo na mirengo yote ya Jamhuri ya Kiislamu yana mtazamo mmoja kuhusu suala hilo.
Kwa upande wao, makamanda na maafisa wote wa kambi ya muqawama walioonana na Kamanda Qaani wameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa uungaji mkono wake kwa wanamapambano hao wa Kiislamu na kwa kuwa kwake mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na waitifaki wake.