Pezeshkian: Iran kamwe haitaliacha taifa la Palestina pekee yake katika vipindi vigumu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i114072-pezeshkian_iran_kamwe_haitaliacha_taifa_la_palestina_pekee_yake_katika_vipindi_vigumu
Rais mteule wa Iran amesisitiza udharura wa kuendelea kuliunga mkono taifa la Palestina dhidi ya utawala ghasibu wa Israel.
(last modified 2024-07-14T23:56:48+00:00 )
Jul 14, 2024 23:56 UTC
  • Pezeshkian: Iran kamwe haitaliacha taifa la Palestina pekee yake katika vipindi vigumu

Rais mteule wa Iran amesisitiza udharura wa kuendelea kuliunga mkono taifa la Palestina dhidi ya utawala ghasibu wa Israel.

Masoud Pezeshkian, rais mteule wa Iran alisema hayo jana katika mazungumzo ya simu na Ismail Haniyeh, Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haitaliacha taifa la Palestina peke yake katika hali na vipindi vigumu.

Katika mazungumzo hayo, rais mteule wa Iran amelaani vikali shambulio la kikatili la hivi karibuni la Israel dhidi ya mkusanyiko wa Wapalestina waliokimbia makazi yao katika kambi ya wakimbizi ya al-Mawasi kusini mwa mji wa Gaza wa Khan Yunis. Mauaji hayo yalisababisha vifo vya Wapalestina zaidi ya 90 na wengine 300 kujeruhiwa.

Al Mawasi, Gaza

Pezeshkian amesema uhalifu huo wa kutisha "unathibitisha hamu ya Israel kuendeleza mauaji ya kimbari na kuvunja azma ya mapambano ya ukombozi ya Wapalestina, lakini kamwe haitafanikiwa."

Amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu haitawaacha watu wa Palestina peke yao katika hali hiyo ngumu.

Kwa upande wake, Ismail Haniyeh ameshukuru uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ajili ya kadhia ya taifa la Palestina na kuiomba Tehran ifanye juhudi zaidi za kisiasa na kidiplomasia za kukomesha hujuma za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza.

Amegusia mauaji ya kutisha yaliyofanywa na Israel dhidi ya raia wa Gaza, yakiwemo mauaji ya al-Mawasi huko Khan Yunis na kusema: Utawala huo ghasibu unatumia madai ya uongo ya eti kuwalenga viongozi wa harakati za ukombozi ili kuhalalisha jinai zake.