Zaidi ya wageni 300 kushiriki hafla ya kuapishwa Rais mpya wa Iran
(last modified Sun, 28 Jul 2024 03:16:04 GMT )
Jul 28, 2024 03:16 UTC
  • Zaidi ya wageni 300 kushiriki hafla ya kuapishwa Rais mpya wa Iran

Zaidi ya wageni 300 watahudhuria hafla ya kuapishwa rais mteule wa Iran Dakta Masoud Pezeshkian.

Duru za karibu kabisa na Bunge la Iran zinasema, zaidi ya jumbe 80 na wageni 300 watahudhuria hafla ya kuapishwa kwa rais mpya wa Iran, mbali na viongozi na maafisa wa ngazi za juu wa ndani.

Wakati huo huo, Mjumbe wa kamati ya maandalizi ya sherehe za kumuapisha Rais ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ametangaza kuwa nchi 60 duniani zimetangaza kuwa zitashiriki katika sherehe za kuapishwa Rais wa Iran wa serikali ya awamu ya 14.

Mojtaba Yousefi ameashiria kufanyika bungeni sherehe za kuapishwa Rais mpya na kusema: Hadi sasa nchi 60 zimetangaza kuwa zitashiriki katika hafla hiyo. Amesema Marais wanne wa nchi, Maspika 12 wa mabunge na Mawaziri Wakuu 7 watahudhuria sherehe za kuapishwa rais mpya wa Iran. 

Rais mteule wa Iran Masoud Pezeshkian

 

Wakati huo, leo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu atantarajiwa kumuidhinisha Rais Mpya Masoud Pezeshkian katika hafla itakayohudhuriwa na maafisa wa kitaifa na kijeshi katika Husseiniya ya Imam Khomeini (MA).

Kisha sherehe za kula kiapo zitafanyika keshokutwa Jumanne tarehe 30 mwezi huu wa Julai katika ukumbi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu saa kumi alasiri kwa wakati wa hapa Tehran kwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na wageni waalikwa kutoka nje ya nchi. 

Dakta Pezeshkian mwenye umri wa miaka 69, alichaguliwa kuwa Rais wa tisa wa Iran baada ya kuibuka na ushindi wa kura milioni 16 na 384,403 kati ya zaidi ya kura milioni 30 zilizopigwa katika duru ya pili ya uchaguzi wa 14 wa Rais wa Iran Ijumaa iliyopita ya Julai 5. Mpinzani wake Saeed Jalili alipata kura 13,538,179. 

Tags