IRGC: Israel isubiri jibu kali la kuumiza kwa kumuua kigaidi Haniyah
Kamanda wa Kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) ameuonya vikali utawala wa Kizayuni wa Israel na kuutaka ujiandae kwa matokeo mabaya na majibu makali ya kuumiza kwa kumuua kigaidi Ismail Haniyah, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS).
Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh amenukuliwa akisema hayo na Iran Press, ambapo ameuhutubu utawala katili wa Israel kwa kuuambia, "Muwe tayari kuwafanya Wazayuni waelewe adhabu kali inayowasubiri kwa kumwaga damu ya mgeni ndani ya ardhi yetu."
Ismail Haniyah na mmoja wa walinzi wake wameuawa shahidi usiku wa kuamkia leo baada ya kushambuliwa makazi yao hapa mjini Tehran, saa chache baada ya kuhudhuria hafla ya kuapishwa kwa Rais mpya wa Iran, Masoud Pezeshkian.
Kamanda wa Kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la SEPAH ameeleza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umetekeleza kitendo cha kikatili cha kumuua shahidi Haniyah katika hali ambayo, taifa la Iran lingali linaomboleza mauaji ya kigaidi ya Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha IRGC.
Wakati huo huo, Idara ya Uhusiano wa Umma ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu imesisitiza pia kuwa, hakuna shaka utawala wa Kizayuni utakabiliwa na jibu kali, zito na la kuumiza kwa kitendo chake cha kumuua shahidi Ismail Haniyah.
Taarifa ya IRGC imebainisha kuwa: Mauaji ya kigaidi ya Haniyah yatakabiliwa na jibu kali na la kuumiza kutoka kwa Mrengo wa Muqawama hasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.