Siasa za serikali ya 14 ya Iran ni kuendeleza ushirikiano mzuri na nchi jirani na za dunia
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa siasa za serikali ya 14 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uga wa siasa za kigeni ni kuwa na maingiliano mazuri na yenye uwiano na nchi jirani na dunia nzima kwa ujumla kwa lengo la kudhamini haki na maslahi ya taifa la Iran.
Rais Masoud Pezeshkian wa Iran, alisema katika hafla ya kuapishwa kwake katika Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) siku ya Jumanne kwamba kipaumbele cha sera za nje za serikali yake kitakuwa ni kuboresha na kuimarisha uhusiano na nchi zote hususan nchi jirani, kwa lengo la kudhamini na kulinda haki na maslahi ya taifa la Iran.
Huku akisisitiza kuwa nchi jirani hazipasi kupoteza rasilimali zao katika mivutano na mashindano yasiyo na maana, Pezeshkian aliongeza kuwa serikali yake itafuatilia juhudi za kujenga eneo lenye nguvu, ambapo nchi zote zitashirikiana katika kufikia maendeleo ya kiuchumi na kuboresha maisha ya baadaye ya watu wa eneo hili. Pezeshkian ambaye alichaguliwa na wananchi tarehe 5 Julai kuwa rais mpya wa Iran katika siku za hivi karibuni amekuwa akizungumza na vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi kuhusu namna serikali yake inavyopanga kuimarisha uhusiano na nchi zote za dunia hususan nchi jirani kwa lengo la kudhamini maslahi ya pande husika.
Ayatullah Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika sherehe za kumuidhinisha Masoud Pezeshkian kuwa rais mpya wa Iran Jumapili (Julai 28), alizungumzia fursa ya Iran kuwa na majirani wengi, na kusisitiza kwamba ni lazima juhudi za dhati zifanyike kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wa Iran na majirani zake. Alisema: "Moja ya vipaumbele muhimu vya sera za kigeni za Iran ni kuimarisha mawasiliano na nchi kama vile za Kiafrika na za Asia, ambayo yanaweza kupanua uwanja wa kidiplomasia wa Iran."
Sisitizo hilo la Kiongozi Muadhamu lina maana kwamba ni muhimu kuendeleza stratijia ya kuwa na uhusiano mzuri na nchi jirani, zenye fikra sawa na za Kiislamu, ambayo ilifuatiliwa katika serikali ya Shahidi Ayatullah Raisi. Matamshi ya Rais Masoud Pezeshkian na ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu siasa na uhusiano wa nje yanaashiria kuwa, siasa za kieneo na kimataifa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika serikali mpya ni mwendelezo wa stratijia ya serikali ya Shahidi Raisi.
Kurejeshwa uhusiano wa Iran na Saudi Arabia na Bahrain na pia kuimarishwa uhusiano wa Iran na nchi za Kiafrika, Asia, Ulaya na Marekani na safari nyingi alizofanya marehemu Raisi katika nchi nyingi ni ushahidi wa juhudi chungu nzima zilizofanywa na serikali yake ya 13 katika kuimarisha uhusiano na nchi jirani na za kimataifa. Iran ina majirani 7 wa mpaka wa nchi kavu na 10 wa mpaka wa majini, jambo ambalo linatoa fursa nyingi za kidiplomasia, kiuchumi na kiutamaduni kwa Iran, na hasa ikitiliwa maanani kuwa utamaduni wa Iran bado una uwepo mkubwa katika nchi nyingi jirani. Kwa kauli ya Rais wa serikali ya 14, katika uga wa siasa za nje, Iran inajaribu kuleta uwiano katika mahusiano yake na nchi zote za ulimwengu kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine, inafuatilia maslahi ya kiuchumi katika siasa zake za kupanua uhusiano na nchi jirani na za nje ya eneo ili kudhamini maslahi ya kiuchumi ya kitaifa.
Hii ina maana kwamba nchi zina haki ya kuchagua washirika na marafiki zao katika pembe tofauti za dunia lakini hazina haki hiyo kuhusiana na majirani zao. Hii ni kutokana na ukweli kwamba jiografia na mambo mengine ya kawaida ya kitamaduni huwa tayari yameziainishia haki hiyo. Kwa hakika uwepo wa mipaka ya kijiografia, kisiasa na kiutamaduni kati ya nchi jirani, tayari huziandalia jukwaa la kushirikiana katika kila nyanja kwa ajili ya maslahi ya pamoja. Hiyo ndio maana nchi jirani zikapewa kipaumbele cha kwanza katika maingiliano na ushirikiano wa nchi yoyote ile na mataifa mengine. Kwa msingi huo hakuna nchi yoyote ikiwemo Iran, ambayo inaweza kufikia malengo yake ya kitaifa katika dunia ya leo bila kuzishirikisha nchi jirani.