Aug 05, 2024 02:31 UTC
  • Ukosoaji wa Iran kwa baadhi ya nchi za Ulaya kwa kuunga mkono vitendo vya kigaidi vya Israel

Ali Bagheri Kani, Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametilia mkazo haki ya kisheria ya Tehran ya kuuadhibu utawala wa Kizayuni; na amelaani na kukemea hatua ya baadhi ya nchi za Ulaya ya kushirikiana na Marekani kuzuia kulaaniwa mauaji ya Kiongozi Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) shahidi Ismail Haniyeh katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Ali Bagheri Kani, Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu, ameyasema hayo katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na Joseph Borrell Mkuu wa  sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya  (EU) alipoashiria kikao maalumu cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichojadili kitendo cha kigaidi cha hivi karibuni cha utawala wa Kizayuni cha kumuua shahidi Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Hamas hapa mjini Tehran na akasema, hatua ya baadhi ya nchi za Ulaya ya kuungana na Marekani katika kuzuia kulaaniwa mauaji hayo na moto wa vita uliowashwa hivi karibuni na Israel huko Yemen na Lebanon itauhamasisha utawala huo kuendelea na vitendo vyake vya kichokozi na vya kinyama na kuhatarisha uthabiti na usalama wa eneo hili.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yazikosoa baadhi ya nchi za Ulaya kwa kuunga mkono utawala dhalimu wa Kizayuni

Bagheri ameashiria athari hasi za kisiasa na kiusalama za jinai hiyo kubwa na akasema, Umoja wa Ulaya unapaswa kutekeleza jukumu na masuulia uliyonayo ya kudumisha amani na usalama wa kimataifa na kuuwekea mashinikizo utawala wa Kizayuni ili kuzuia kuendelea jinai za utawala huo ghasibu.

Licha ya kimya cha Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya kuhusiana na jinai ya hivi karibuni ya utawala wa Kizayuni ya kumuua shahidi Ismail Haniyeh kiongozi wa kisiasa wa harakati ya Hamas hapa mjini Tehran na kutochukua hatua yoyote nchi hizo kuhusiana na jinai hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani jinai hiyo ya kigaidi na akasisitiza katika mazungumzo na Ali Bagheri kwamba kulingana na sheria za kimataifa, Iran ina haki ya kujihami kisheria na kujilinda dhidi ya ukiukaji wa usalama wake wa taifa na umoja wa ardhi yake.

Guterres ameeleza wasi wasi alionao kutokana na chokochoko za hivi karibuni za utawala wa Kizayuni katika eneo na akasema ana hofu juu ya uwezekano wa kutokea vita kamili katika eneo na matokeo hasi ya vita hivyo.

Ismail Haniyeh, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, aliuawa shahidi alfajiri ya kuamkia Jumatano iliyopita tarehe 31 Julai 2024 katika shambulio lililolenga jengo la makazi aliyofikia kaskazini mwa Tehran.

Shahidi Ismail Haniyeh Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) alikuwa mwanamapambano ambaye alijitolea maisha yake yote katika kuendesha mapambano dhidi ya maadui wa Uislamu

Viongozi wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamesema, utawala wa Kizayuni ulivuka mstari mwekundu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kumuua shahidi Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas mjini Tehran, na wamesisitiza kuwa jibu la Iran kwa jinai hiyo litakuwa kali.

Kuhusiana na suala  hilo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (SEPAH) lilisisitiza katika taarifa yake ya siku ya Jumamosi kwamba kulipiza kisasi cha damu ya Shahidi Ismail Haniyeh ni hatua ambayo utekelezaji wake hauna shaka yoyote na utawala afriti na wa kigaidi wa Kizayuni utapata jibu kali la jinai hiyo ambayo ni "adhabu kali" itakayotolewa katika mahali na wakati mwafaka na kwa namna inayostahiki.

Katika siku za hivi karibuni, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetumia uwezo wake wote wa kidiplomasia, ikiwa ni pamoja na kuitisha kikao maalumu cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kikao maalumu cha nchi za Kiislamu, ikitaka zichukuliwe hatua za kuzuia kuendelea jinai za Wazayuni katika eneo.

Kutokubaliana jinsi ya kukabiliana na mashambulizi  makali ya Iran: Maafisa wa zamani na wa sasa

Lakini sambamba na juhudi hizo za kidiplomasia, imetangaza wazi kuwa imeshajiandaa kutoa jibu kwa jinai ya karibuni ya Wazayuni.

Kuhusiana na hilo, ushahidi uliopo unaonyesha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, -kwa kuzingatia msingi wa haki halali na ya kisheria ya kujihami kulingana na sheria za kimataifa-, imeshachukua hatua za utangulizi zinazohitajika kwa ajili ya kutoa jibu la mauaji ya kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh yaliyofanywa hapa mjini Tehran; na jibu hilo litakuwa na wigo mpana zaidi na la uharibifu mkubwa zaidii kuliko operesheni ya "Ahadi ya Kweli" iliyotekelezwa baada ya shambulio la Wazayuni kwenye ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mji mkuu wa Syria, Damascus mwezi Aprili mwaka huu.

 

Tags