Khatibu wa Sala ya Ijumaa: Utawala wa Kizayuni ujue kwamba tutalipiza kisasi cha damu ya Shahidi Ismail Haniya
Aug 09, 2024 12:02 UTC
Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran amesisitiza ulazima wa kulipiza kisasi cha damu ya Shahidi Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina, HAMAS.
Haniya na mmoja wa walinzi wake waliuawa shahidi alfajiri ya kuamkia Jumatano ya tarehe 31 Julai kutokana na shambulio la kigaidi lililofanywa mjini Tehran.
Kwa mujibu wa IRNA, Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami amesema katika Sala ya Ijumaa ya wiki hii mjini Tehran kwamba, utawala wa Kizayuni na Marekani wanahusika katika jinai za Ghaza na kuuawa shahidi Ismail Haniya na akabainisha kuwa, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametumia msamiati maalumu kuhusu kuuawa shahidi kiongozi huyo wa Hamas aliposema, ni wajibu kwetu kulipiza kisasi cha damu ya Mujahidina huyo; na kwa hivyo utawala wa Kizayuni ujue kwamba tutalipiza kisasi cha damu ya Shahidi huyo.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran ameongezea kwa kusema: “lakini sisi tuna Mfumo wenye mpangilio, kwa hiyo mpangilio wetu utaamua tupige lini, wapi na vipi; na utawala wa Kizayuni utabaki muda wote kuwa na hofu na kiwewe hadi wakati huo, lakini ujue kwamba, tutalipiza kisasi kwa wakati na mahali mwafaka."
Akizungumzia kuuawa shahidi Ismail Haniya mjini Tehran, Ayatullah Khatami amesema: "jinai hiyo na jinai zinazofanywa huko Ghaza zinaonyesha kuwa utawala wa Kizayuni ni muuaji, fisadi na mharibifu, na ni haki kuutolea utawala huo kaulimbiu ya 'Mauti kwa Israel'. Na hapana shaka pia kwamba, jinai zilizofanywa na Wazayuni kwa zaidi ya miezi 10 sasa huko Ghaza zinafanywa chini ya usimamizi wa Marekani; na lau utawala huo wa kibeberu usingewaunga mkono wahalifu hao wa Kizayuni, Wapalestina zaidi ya 40,000 wasingekuwa wameuawa shahidi".
Khatibu wa Sala ya Ijumaa ameashiria pia kuchaguliwa Yahya Sinwar kuwa Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas na akasema: kuchaguliwa Sinwar ni sawa na kuuzaba kibao utawala wa Kizayuni.
Ayatullah Khatami amekumbusha kuwa Sinwar alifungwa jela na Wazayuni kwa zaidi ya miaka 20 lakini aliwaambia Wazayuni kuwa, iko siku sisi tutakuchukueni nyinyi mateka.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Khatibu wa muda wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran amelitaka Bunge na Serikali zizingatie vigezo alivyotoa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kuchagua mawaziri wa serikali ya 14 na kusisitiza kuwa, kuundwa Baraza la Mawaziri ambalo mawaziri wake ni watu waaminifu, wakweli, washikadini, wasafi na wachapakazi ni kwa manufaa ya Mfumo wa Kiislamu.../