Jumanne, 09 Septemba, 2025
Leo ni Jumanne tarehe 16 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1447 Hijria sawa na tarehe 09 Septemba 2025.
Siku kama ya leo miaka 1453 iliyopita kulianza vita maarufu kwa jina la vita vya miaka saba kati ya madola mawili yaliyokuwa na nguvu ya Iran na Roma, baada ya mfalme Justinian wa Roma kuanzisha mashambulizi yaliyokuwa na lengo la kulikalia eneo la magharibi mwa Iran.
Baada ya miaka saba ya vita mfalme wa Iran Anushirvan alimshinda mfalme Justinian wa Roma na hivyo mfalme huyo akalazimika kujiuzulu. Baada ya kujiuzulu Justinian, mfalme Tiberius alishika mamlaka ya utawala wa Roma.
Vita hivyo vilimalizika mwaka 579 baada ya Waroma kukubali kuilipa Iran gharama inayofikia sarafu za dhahabu elfu 45.

Siku kama ya leo miaka 1446 kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, Swala ya kwanza ya Ijumaa iliswaliwa na Mtume Muhammad (saw) baada ya mtukufu huyo kuhama mji wa Makka.
Baada ya kuwasili katika eneo la Bani Salim bin Auf kwa jina la Quba karibu na Madina wakati wa adhuhuri, Mtume (saw) alitoa hotuba na kusimamisha Swala ya Ijumaa mahala hapo. Wanahistoria wanasema hiyo ilikuwa Swala ya kwanza ya Ijumaa katika Uislamu.
Hatua hiyo pia inaonesha umuhimu wa ibada hiyo ya kiroho na kisiasa ambayo Bwana Mtume aliamua kuitekeleza mara tu baada ya kuwasili karibu na mji wa Madina. Baadaye Waislamu walijenga msikiti katika eneo hilo palipofanyika Swala ya Ijumaa ya kwanza katika Uislamu.

Katika siku kama hii ya leo miaka 197 iliyopita alizaliwa Leo Tolstoy, mwandishi na mwanafasihi raia wa Russia.
Awali Tolstoy alijiunga na jeshi la Qaukasia na katika kipindi hiki ndipo alipoandika kitabu chake cha kwanza alichokupa jina la "Childhood". Mwandishi huyo wa Russia baadae alijiengua jeshini na kutumia muda wake wote kwa ajili ya kusoma na kuandika.
Miongoni mwa vitabu muhimu vya mwandishi Leo Tolstoy ni "Vita na Amani", "Waqazaki" na "Hadji Murad." Tolstoy alifariki dunia mwaka 1910.

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita yaani tarehe 9 Septemba 1945, ulitiwa saini mkataba wa kusalimu amri vikosi vya Japan vilivyokuwa vimeidhibiti na kuikalia kwa mabavu China. Kwa mujibu wa mkataba huo askari milioni moja wa Japan waliweka chini silaha zao kwa amri ya Hirohito mfalme wa wakati huo wa Japan. Kwa utaratibu huo vita vya kihistoria kati ya China na Japan vikafikia tamati.

Siku kama ya leo miaka 49 iliyopita, aliaga dunia Mao Zedong kiongozi wa Uchina.
Mao Zedong alizaliwa mwaka 1893 na mwaka 1921 aliunda chama cha Kikomonisti cha Uchina baada ya kuungwa mkono na wafuasi wa fikra zake.
Mao alikuwa akisisitiza suala la kuwatetea na kuwalinda wanavijiji na kwa sababu hiyo ilipata uungaji mkono mkubwa wa wanavijiji wa Uchina.
