Aug 10, 2024 13:43 UTC
  • Iran: Tumeshaandaa mazingira ya kutoa jibu kali dhidi ya Israel

Mshauri wa masuala ya kisiasa wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei amesema mazingira yameshaandaliwa kwa ajili ya Iran kutoa jibu kali na la kuumiza dhidi ya Israel, kutokana na hatua ya utawala huo wa Kizayuni kumuua shahidi Ismail Haniyah, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS.

Admeri Ali Shamkhani amesema hayo leo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X na kuongeza kuwa: Michakato ya kisheria, kidiplomasia na vyombo vya habari imeandaa uwanja wa kuadhibiwa vikali utawala ambao unaelewa tu lugha ya mabavu. 

Haniyah na mmoja wa walinzi wake waliuawa shahidi alfajiri ya kuamkia Jumatano ya tarehe 31 Julai hapa mjini Tehran, siku moja baada ya kuhudhuria hafla ya kuapishwa Rais mpya wa Iran, Masoud Pezeshkian.

Admeri Shamkhani amebainisha kuwa, lengo hasa la utawala wa Kizayuni kuwaua shahidi waumini wa Kiislamu katika shule ya al-Tabieen huko Gaza, na kumuua kigaidi Ismail Haniyah nchini Iran, ni kutaka vita na kufelisha mazungumzo ya usitishaji vita (katika Ukanda wa Gaza).

Wakati huo huo, Naibu Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) amesema amri iliyotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei juu ya kulipiza kisasi cha damu ya Shahidi Haniyah ipo wazi na bayana.

Brigedia Jenerali Ali Fadavi

Brigedia Jenerali Ali Fadavi amesema hayo leo na kuongeza kuwa, agizo la Kiongozi Muadhamu la kuadhibiwa utawala wa Kizayuni kwa jinai zake litatekelezwa kwa wakati mwafaka.

Naye Brigedia Jenerali Ali Mohammad Naeeni, Msemaji wa Ofisi ya Uhisiano Mwema ya SEPAH amesema lengo la utawala wa Kizayuni la kumuua kigaidi Ismail Haniyah, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS ni kuibua mifarakano baina ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na Sunni.

Tags