Aug 14, 2024 12:30 UTC
  • Kiongozi Muadhamu atilia mkazo wajibu wa kusimama imara mbele ya vita vya kisaikolojia vya adui

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametilia mkazo wajibu wa kusimama imara kukabiliana na vita vya kisaikolojia vya adui akisema kuwa, wanaoendesha vita hivyo dhidi ya Iran wanajaribu kuzusha hofu na kulifanya taifa hili lilegeze kamba na lirudi nyuma katika nyuga tofauti.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo Jumatano wakati alipoonana na maafisa na wakuu wa Kamati ya Baraza la Taifa la Mashahidi la mkoa wa Kohgiluyeh na Boyer-Ahmad akisisitiza kuwa, moja ya misingi mikuu ya vita vya kisaikolojia dhidi ya taifa azizi la Iran ya Kiislamu ni kujaribu kuonesha kuwa maadui wana uwezo na nguvu kubwa. Amesema, tangu mwanzoni kabisa mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hadi hivi sasa, maadui wamekuwa wakitumia njia tofauti kujaribu kulitia hofu taifa la Iran na kujaribu kuonesha kuwa lazima wananchi wetu waiogope Marekani, Uingereza na utawala wa Kizayuni.

Vile vile amesema kuwa, lengo la adui la kuzusha vita vya kisaikolojia katika upande wa masuala ya kijeshi ni hilo hilo la kuzitia hofu nyoyo za wananchi wa Iran lakini kama inavyotufundisha Qur'ani Tukufu, kurudi nyuma na kulegeza kamba kizembe katika medani yoyote iwe ya kijeshi au medani nyingine za kisiasa, kipropaganda na kiuchhumi, kunaendana na ghadhabu za Mwenyezi Mungu.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

 

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei pia amesema kuwa, lengo la adui kujifanya mkubwa katika medani ya utamaduni pia ni kujaribu kuyafanya mataifa mengine yachukue hatua za pupa na yakubali kutekwa na utamaduni wa adui na kudharau ustaarabu wao. Matokeo mabaya ya jambo hilo ni kuiga mtindo wa maisha wa adui na hata kutumia misamiati ya wageni katika maisha ya kila siku ya taifa fulani.

Vile vile amesema kuwa, inabidi wapongezwe wale vijana ambao wamesimama imara bila ya woga wala kuathiriwa na maneno ya wengine mbele ya vita hivyo vya kisaikolojia na inabidi uhakika huo ushuhudiwe pia katika kazi za kisanii na kiutamaduni na kwenye nyuga nyinginezo.

Tags