Iran yaapa kuendelea kuimarisha uwezo wake wa kujihami
Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Brigedia Jenerali Hossein Dehqan amesema Jamhuri ya Kiislamu imeazimia kuimarisha uwezo wake wa kujihami na kuzuia maadui.
Akizungumza Jumanne mjini Tehran wakati wa kupokea helikopta nne zilizotengenezwa na pia zilizokarabatiwa katika viwanda vya Wizara ya Ulinzi ya Iran, Brigedia Jenerali Dehqan ameongeza kuwa, Iran kamwe haitababaishwa na vita vya kisaikolojia vya adui.
Ameongeza kuwa, Wizara ya Ulinzi ya Iran ina mpango kabambe wa kuhakikisha kuwa vikosi vyote vya kijeshi nchini vinajiimarisha kikamilifu. Brigedia Jenerali Dehqan ameongeza kuwa wataalamu wa kijeshi wa Iran wana uwezo wa hali ya juu katika kukidhi mahitaji ya kiulinzi nchini.
Katika siku za hivi karibuni baadhi ya maafisa wa nchi za Magharibi wamejaribu kufungamanisha mpango wa makombora ya kujilinda ya Iran na yale mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji JCPOA baina ya Iran na madola sita makubwa duniani.
Ban Ki-moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa ripoti na kudai, hatua ya Iran ya kufanya majaribio ya makombora ya balistiki ni 'jambo linalokiuka moyo' wa mapatano ya nyuklia ambayo yanajulikana rasmi kama 'Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA)'. Akijibu ripoti hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema, "Ripoti hiyo imetayarishwa kwa kutegemea taarifa ambazo si kamili na inaonyesha jinsi Katibu Mkuu wa UN asivyoelewa mazungumzo ya nyuklia."
Iran imesisitiza mara kadhaa kuwa maudhui ya mpango wake wa kujilinda, hasa kuhusu makombora, haiko hata kidogo katika mapatano ya nyuklia.