Pezeshkian afafanua mipango ya serikali yake katika mazungumzo na wananchi
-
Rais Masoud Pezeshkian
Katika mazungumzo yake ya kwanza ya televisheni na wanachi, Rais Masoud Pezeshkian amefafanua mipango ya serikali yake katika nyanja za ndani na nje ya nchi, na kusema kuwa vipaumbele vya serikali ya 14 ni kuwaridhisha wananchi, kuzingatia masuala ya kiuchumi na kuimarisha uhusiano na nchi mbalimbali.
Akizungumza Jumamosi usiku, mazungumzo hayo yaliyorushwa moja kwa moja kupitia televisheni na redio ya taifa, Rais Pezeshkian amesema kuwa kuimarisha umoja wa kitaifa, kuridhisha na kuboresha hali ya kiuchumi ya wananchi na vilevile kudhamini maslahi ya taifa ndilo lengo muhimu zaidi la serikali yake katika uwanja wa ndani. Rais amesisitiza kuwa ikiwa ni katika kutekeleza ahadi alizotoa kwa wananchi na mfumo wa Kiislamu na kama alivyosema katika kampeni za uchaguzi, ameunda serikali itakayofuatilia kuimarisha umoja wa kitaifa ambayo inajumuisha shakhsia na wasomi kutoka mirengo na makundi yote ya kisiasa na kijamii nchini.
Huku akiashiria kwamba Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya zimewawekea mazingira magumu na vikwazo wananchi Iran kwa kisingizio cha mpango wa amani wa nyuklia wa Iran, Rais Pezeshkian amesema serikali inafanya juhudi za kupunguza makali ya vikwazo hivyo kwa kutegemea umoja wa wananchi na kuimarisha uhusiano na nchi jirani, za eneo na rafiki.
Mwezi mmoja ukiwa umepita tangu serikali ya 14 ya Iran inayoongozwa na Rais Masoud Pezeshkian iingie madarakani, kuchaguliwa watu tofauti kwa ajili ya kuongoza wizara, mashirika na idara za utendaji bila kujali kabila, jinsia na madherhebu ya wahusika bali kwa kuzingatia tu uwezo na uaminifu wao kwa mfumo wa Kiislamu, kunaonyesha wazi kuwa rais ameheshimu na kutekeleza nara na ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi za kuimarisha umoja wa wananchi kwa ajili ya kufikia malengo makuu ya taifa. Katika midahalo ya uchaguzi huo, Pezeshkian alisema mara kadhaa kwamba kuendeshwa nchi na kutekelezaji mipango mikuu ya taifa katika sekta za siasa, uchumi na masuala ya kijamii hakuwezi kutekelezeka bila kutumiwa uwezo wote wa nchi na nguvukazi stahiki. Kwa mtazamo huu, kuwepo mwafaka wa kitaifa kwa shabaha ya kuimarisha umoja na mshikamano wa ndani ni kanuni ambayo inapasa kufuatiliwa na wananchi na viongozi wote.
Juhudi za kuimarisha umoja na kunufaika na mitazamo ya makundi tofauti nchini ni moja ya amri muhimu za dini tukufu ya Kiislamu, ambayo imesisitizwa mara nyingi katika kitabu cha mbinguni cha Waislamu (Qur'an Tukufu). Ni kwa msingi huo ndipo Rais Pezeshkian akasisitiza katika mazungumzo yake ya kwanza na wananchi kupitia televisheni kuwa ufunguo wa kutatuliwa matatizo ya wananchi katika nyanja mbalimbali ni kuimarisha mafungamano ya ndani na kutatuliwa tofauti zilizopo nchini. Suala jingine ambalo rais alilisisitiza katika mazungunzo ya Jumamosi usiku ni kuimarisha uhusiano na nchi zote za dunia, hasa nchi jirani, za kanda na rafiki, suala ambalo amekuwa akiliashiria mara kwa mara katika wiki za hivi karibuni. Safari anayotazamiwa kuifanya Rais Pezeshkian hivi karibuni nchini Iraq na huko New York kwa ajili ya kukushiriki katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo atakutana na viongozi wa nchi mbalimbali kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa pande mbili inatathminiwa katika mtazamo huo.
Akizungumza mwezi uliopita wakati wa kuapishwa kwake bungeni, Rais Pezeshkian alizitaka nchi jirani zisipoteze rasilimali zao katika mivutano na mashindano ya kupimana nguvu bali zichukue hatua kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na uboreshaji wa maisha ya raia wao. Amesema Iran inajaribu kuleta uwiano katika mahusiano yake na nchi zote katika uga wa siasa za nje, na wakati huo huo kudhamini maslahi yake ya kiuchumi kwa kupanua uhusiano na nchi zote, zikiwemo nchi jirani na za nje ya eneo hili. Kwa hakika, siasa za ujirani mwema zinazojikita katika kuimarisha diplomasia ya uchumi, kuongeza maingiliano na majirani, kunufaika na uwezo wao katika kuimarisha mahusiano katika nyanja zote na kupunguza mivutano kati yao ni moja ya sera muhimu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambazo hazibadiliki kwa kubadilika serikali na viongozi wanaoingia madarakani katika vipindi tofauti vya utawala.