Rekodi mpya katika uzalishaji wa umeme wa nyuklia nchini Iran
Kiwanda pekee cha nishati ya nyuklia cha Iran kilifikia kiwango cha uzalishaji cha zaidi ya saa bilioni 7 za kilowati katika mwaka huu wa Hijria Shamsiya.
Hayo yamedokezwa na Mohammad Eslami mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI).
Akizungumza Jumapili amesema kwamba Kiwanda cha Nyuklia cha Bushehr, kilichoko kusini mwa Iran kwenye pwani ya Ghuba ya Uajemi, kimetangazwa kuwa miongoni mwa vinu vinane bora zaidi vya kuzalisha nishati ya nyuklia duniani mwaka jana katika masuala ya ufanisi na usalama.
Eslami, ambaye alikuwa akitoa maelezo kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Iran ya Mpango, Bajeti na Ukaguzi, alisema kuwa umeme unaozalishwa katika kiwanda cha nyuklia cha Busher katika kipindi cha miaka 10 iliyopita ulikuwa na thamani mara mbili ya uwekezaji wa serikali katika ujenzi wa kituo hicho cha umeme.
Amesema Iran inafuatilia kwa karibu mipango ya kujenga vinu vipya vya nyuklia kaskazini na kusini kutokana na viwango vya juu vya ufanisi vilivyopo katika sekta hiyo.
Eslami amesema moja ya mitambo mipya ya nishati ya Iran itakuwa ni kujenga kiwanda cha kuzalisha megawati 300 ambacho kitajengwa na mashirika ya Iran.
Amebaini kuwa Shirika la Nishati ya Atomiki la Irani ina mipango mingi ya kuimarisha uchimbaji wa madini ya urani ambayo ni muhimu katika uzalishaji nishati ya nyuklia.