Rais Pezeshkian: Jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel hazitabaki bila kujibiwa
Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema ni lazima Tehran itoe jibu kwa utawala unaotenda jinai wa Israel.
Akihutubia kikao cha baraza la mawaziri siku ya Jumapili, Rais Pezeshkian kwa mara nyingine tena amelaani vikali kitendo cha Israel cha kumuua kigaidi Sayyid Hassan Nasrallah, kiongozi wa Hizbullah ya Lebanon, katika shambulio kubwa la anga katika eneo la kusini mwa Beirut siku ya Ijumaa kwa kutumia mabomu yenye nguvu kubwa yaliyotoka Marekani.
Amesema: "Jinai hii kwa mara nyingine imetibitisha kwamba utawala huu utendao jinai hauzingatii kanuni na sheria zozote za kimataifa."
Ameongeza kuwa vitendo vya uhalifu vya Israel "havikubaliki" na havitapita bila kujibiwa. Aidha amesisitiza kuwa uzoefu wa kihistoria unaonyesha kuwa mauaji ya viongozi wa harakati za kupigania uhuru hayawezi kusitisha harakati hizo.
Amesema: "Watu wengi zaidi wako tayari kuinua bendera ya kutetea haki na kupinga dhuluma." Ameongeza kuwa, kwa kutochukua hatua dhidi ya uhalifu unaofanywa na Israel, Marekani na washirika wake wanashajiisha Israel kufanya vitendo zaidi vya jinai.
Rais Pezeshkian amesisitiza umuhimu wa kuwaunga mkono wapiganaji wa Hizbullah katika vita vyao na Israel ili kuuzuia utawala huo ghasibu kuzishambulia nchi za mhimili wa muqawama na kuua wanawake na watoto wasio na hatia.
Amesisitiza uwajibikaji mzito wa nchi za Kiarabu na Kiislamu katika kukabiliana na hujuma za kikatili za utawala wa Israel katika eneo.
Rais wa Iran pia amevilaumu vyombo vya habari vya Magharibi kwa kupuuza na kunyamazia kimya ugaidi wa Israel na 'kukukuza matukio madogo zaidi nchini Iran".
Aidha amesema Wizara ya Afya ya Iran na mashirika yote ya misaada yamejiandaa kikamilifu kuwasaidia wahanga wa mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel dhidi ya Lebanon.