Onyo la Iran kwa waungaji mkono wa Israel; Kaeni mbali na vita
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amezionya nchi za Magharibi na waungaji mkono wengine wa Israel katika eneo dhidi ya kuingilia mzozo kati ya Jamhuri ya Kiislamu na utawala wa Kizayuni.
Amir Saeid Iravani ametoa indhari hiyo katika mahojiano na chombo kimoja cha habari cha Marekani, alipoulizwa kuhusu kina cha jibu la Iran mkabala wa shambulio tarajiwa la Israel dhidi ya Iran, baada ya Tehran kuinyeshea Tel Aviv kwa mvua ya makombora ya balestiki kulipiza kisasi cha damu za viongozi na makamanda wa ngazi za juu wa mrengo wa Muqawama.
Iravani amebainisha kuwa, "Jibu letu litamlenga tu mvamizi. Iwapo kuna nchi itamsaidia mvamizi, itatambuliwa kama mshirika wa jinai, na itakuwa shabaha halali (ya Iran)."
Amesisitiza kuwa, shambulio la makombora ya balistiki la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel la Jumanne lilikuwa jibu la lazima kwa vitendo vya kigaidi vya utawala huo ghasibu katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.
Balozi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema Israel inalisukuma eneo la Asia Magharibi katika ukingo wa janga kubwa ambalo halijawahi kutokea.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameeleza bayana kuwa: Ushauri wetu (kwa nchi za Magharibi na waungaji mkono wengine wa Israel katika eneo) ni kwamba, msijiingize katika mzozo baina ya utawala wa Israel na Iran, mkae mbali kabisa na vita.