Ziara ya Araghchi nchini Syria kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kikanda wa Iran
(last modified Sun, 06 Oct 2024 14:24:43 GMT )
Oct 06, 2024 14:24 UTC
  • Ziara ya Araghchi nchini Syria kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kikanda wa Iran

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika muendelezo wa ziara yake ya kieneo ametembelea pia Damascus, mji mkuu wa Syria kukutana na kushauriana na viongozi wa ngazi za juu wa nchi hiyo.

Sayyid Abbas Araghchi, ambaye anaongoza ujumbe wa juu wa kisiasa wa Iran, jana Jumamosi Oktoba 5, alionana na Rais Bashar al Assad mjini Damascus na Waziri Mkuu wa Syria Mohammad Ghazi al-Jalali. Katika mazungumzo yao, Rais Bashar al Assad na Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamejadiliana njia za kukomesha mashambulizi ya kinyama na ya kichokozi ya utawala katili wa Israel dhidi ya Lebanon, na njia za kuwasaidia na kuwafikishia misaada wananchi wa Lebanon katika ngazi ya kiserikali na ya watu wa kujitolea. Viongozi wa makundi ya muqawama ya Palestina pia, wamekutana na Araghchi mjini Damascus, Syria.

Katika mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Rais Bashar al Assad amepongeza misimamo ya kuwajibika na imara ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, katika kuwatetea wananchi madhulumu wa Palestina na uungaji mkono wake madhubuti na wa kisheria wa kupigania haki ya kujitawala na kujihami wananchi kama ambavyo ametilia mkazo poia umuhimu wa kufanyika juhudi za kila upande za kupambana na uvamizi wa adui Mzayuni. Kwa upande wake Araghchi, pia amesisitizia suala la kuendelea uungaji mkono wa pande zote wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa Syria na Muqawama wa kukabiliana na uvamizi wa kinyama  na uchochezi wa utawala wa Kizayuni.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Rais wa Syria

Kabla ya safari yake ya kwenda Damascus Syria, Araghchi alienda Beirut, mji mkuu wa Lebanon, kukutana na kushauriana na viongozi wa nchi hiyo na kujadiliana nao hali inayoendelea hivi sasa katika ukanda huu. Awamu hii mpya ya ziara ya Araghchi ya kuzitembelea nchi za eneo hili imefanyika wakati huu ambapo utawala wa Kizayuni unafanya mashambulizi ya kivamizi na ya kinyama dhidi ya Lebanon, Syria na Palestina.

Katika siku za hivi karibuni, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran alishiriki katika kikao cha pamoja na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi. Katika kikao hicho, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wa nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi walijadiliana hali iliyopo hivi sasa katika ukanda huu na masuala ya kimataifa, yakiwemo ya Palestina na Lebanon na walitilia mkazo wajibu wa kuweko maelewano na ushirikiano wa nchi za eneo hili kwa ajili ya kutatua migogoro na changamoto zilizopo. 

*** Katika siku za hivi karibuni, utawala wa Kizayuni umekuwa ukiishambulia mara kwa mara Beirut na baadhi ya maeneo ya Syria kinyume na sheria, na mashambulizi hayo ya Wazayuni yanafanyika kwa uratibu kamili na serikali za Washington na  nchi za Wamagharibi.

Katika hali kama hiyo, safari ya Araghchi katika eneo hilo  inahesabiwa kuwa ni duru mpya ya mashauriano na juhudi za Jamhuri ya Kiislamu ya  Iran kwa ajili ya uratibu na ushirikiano zaidi na nchi ambazo ziko mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni. Ushirikiano na mshikamano wa nchi za eneo la Magharibi mwa Asia unaweza kuwa na nafasi muhimu katika kusimama kidete kukabiliana na uchochezi wa utawala wa Kizayuni. 

Araghchi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria

Utawala katili wa Israel unatiwa wasiwasi zaidi na ushirikiano na umoja wa nchi zenye taathira katika eneo la Asia Magharibi, na Wazayuni wanajua vyema kwamba, kuongezeka kwa ushirikiano huo kutaimarisha makundi ya Muqawama kwa ajili ya kukabiliana na sera za vita na uvamizi wa Israel.

Duru mpya ya safari ya Araghchi inaonyesha utayarifu wa nchi za eneo hilo kwa ajili ya ushirikiano kuhusu Palestina na Lebanon. Mashauriano ya kieneo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Sayyid Abbas Araghchi, pia yanaashiria kuongezeka hali ya kuaminiana kati ya maafisa wa nchi za eneo la Asia Magharibi na kutoathiriwa kwao sera za vita za utawala wa Kizayuni. Ushirikiano wa kikanda na kuzuia uingiliaji wa kigeni daima umekuwa sehemu ya isiyobadilika ya sera  za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na matunda yake yamevutia hisia za nchi za eneo hilo.