Iran: Tumejiweka tayari kikamilifu kulinda mamlaka ya utawala ya ardhi yetu
(last modified Fri, 11 Oct 2024 07:46:40 GMT )
Oct 11, 2024 07:46 UTC
  • Iran: Tumejiweka tayari kikamilifu kulinda mamlaka ya utawala ya ardhi yetu

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imejiweka tayari kikamilifu kulinda mamlaka yake na umoja wa ardhi yake dhidi ya uvamizi na uchokozi wowote utakaoyalenga maslahi yake makuu na usalama wake.

Amir Saeed Iravani, ameyasema hayo katika kikao cha Baraza la Usalama kilichojadili hali ya Lebanon na akafafanua kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitaki kuanzisha vita wala kuzidisha mivutano katika eneo, lakini itatumia kwa uwezo wake wote haki yake ya uhalali wa kulinda mamlaka yake ya utawala na umoja wa ardhi yake dhidi ya uchokozi wowote kwa mujibu wa sheria za kimataifa na italijuulisha Baraza la Usalama kuhusu jibu lake itakalotoa kulingana na sheria.
 
Mwanadiplomasia huyo mwandamizi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ametahadharisha pia kuhusu hali mbaya ya kibinadamu nchini Lebanon na akawahutubu wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa akisema: "itibari ya Baraza hili iko hatarini na Baraza la Usalama linapaswa kuuwajibisha utawala wa Israel kwa kufanya mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya watu wa Lebanon na Palestina".
Amir-Saeed Iravani

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, utatuzi wa haki wa mgogoro huo unahitaji kutambuliwa mamlaka na uhuru wa Lebanon, kukomeshwa uvamizi haramu na uchokozi wa utawala haramu wa Israel sambamba na kuheshimiwa sheria za kimataifa na Hati ya Umoja wa Mataifa.

 
Iravani amesisitizia pia ulazima wa kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Ghaza na kuendelezwa juhudi za Jamii ya Kimataifa na Baraza la Usalama ili kufikia lengo hilo.
 
Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni amepanua vita vya uvamizi hadi Lebanon na Syria baada ya mauaji ya kimbari yaliyodumu kwa mwaka mmoja dhidi ya Wapalestina wa Ghaza.../