Ahmad Nourozi apongeza uungaji mkono wa Afrika Kusini kwa wananchi wa Palestina
Mkuu wa kitengo cha matangazo ya nje cha Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) amesema kuwa Afrika Kusini inang'aa kama nyota katika kuwaunga mkono na kuwatetea wananchi wa Palestina na imekuwa na mchango athirifu katika uwanja huo.
Ahmad Nourozi ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Sehloho Francis Moloi, balozi wa Afrika Kusini nchini Iran na kuashiria hatua za pamoja za nchi mbili katika kupambana na dhulma na ubeberu duniani.
Nourozi amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inashikamana na mapambano ya Afrika Kusini dhidi ya ubeberu duniani kwa ajili ya kuikomboa nchi hiyo kutoka katika makucha ya ubaguzi wa Apartheid.
Mkuu wa Kitengo cha Matangazo ya Nje cha IRIB pia amekumbusha kesi iliyofunguliwa na Afrika Kusini katika mahakama ya ICJ dhidi ya Israel kufuatia mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala huo dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza na kusisitiza kuwa: Dunia inapasa kuona aibu kutokana na matukio yanayoendelea kushuhudiwa katika Ukanda wa Gaza na vilevile huko kusini mwa Lebanon kwa sababu imenyamaza kimya bila kuchukua hatua mkabala wa jinai za utawala wa Kizayuni.
kwa upande wake, balozi wa Afrika Kusini nchini Iran ameashiria uhusiano mwema kati ya nchi mbili na kusema, uhusiano huu uliasisiwa kutokana na mapambano ya haki na uhuru, na Afrika Kusini inathamini nafasi na mchango mkubwa wa Iran katika kusaidia mapambano ya watu wa Afrika Kusini kwa ajili ya kujikomboa dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi na ukoloni.
Balozi wa Afrika kusini pia amezitaja jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na nchini Lebanon kuwa ni migogoro mikubwa inayoikabili dunia sasa na kusema, Iran na Afrika Kusini zinapasa kuliwasilisha suala hili katika taasisi za kimataifa ili kuzuia mauaji ya kimbari ya Wazayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.