Iran na Sudan zajadili uhusiano na masuala ya kiuchumi
(last modified Sat, 09 Nov 2024 13:25:08 GMT )
Nov 09, 2024 13:25 UTC
  • Iran na Sudan zajadili uhusiano na masuala ya kiuchumi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amekutana na Waziri wa Fedha na Mipango ya Kiuchumi wa Sudan, Gibril Ibrahim Mohamed, aliyeko safarini mjini Tehran kujadili uhusiano wa pande mbili, biashara na uchumi.

Maafisa hao wawili wamekaribisha kurejeshwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya Tehran na Khartoum na kueleza matumaini kwamba ukurasa huo mpya utaimarisha ustawi wa uchumi na biashara kati ya mataifa hayo mawili.

Pande hizo mbili pia zimesisitiza utayarifu wa serikali za Iran na Sudan kupanua uhusiano katika nyanja mbalimbali.

Waziri wa Fedha na Mipango ya Kiuchumi wa Sudan, Gibril Ibrahim Mohamed, ambaye yuko Tehran akiongoza ujumbe wa kiuchumi wa serikali ya Khartoum, Jumatano iliyopita pia alifanya mazungumzo na Waziri wa Masuala ya Uchumi na Fedha wa Iran Abdolnaser Hemmati.

Katika mazungumzo hayo, Ibrahim Mohamed litaja faida kama vile kuwepo kwa ardhi yenye rutuba nchini Sudan kwa ajili ya mazao ya kilimo, ikiwa ni pamoja na mbegu za mafuta, ufuta, karanga, pamoja na ufugaji na rasilimali nyingi za chini ya ardhi kuwa vinaifanya Sudan kuwa mojawapo ya fursa za uwekezaji. Gibril Ibrahim Mohamed pia alieleza hamu ya serikali na watu wa Sudan ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kiuchumi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Inafaa kuashiria kuwa Jamhuri ya Sudan ina eneo la kilomita za mraba 1,886,000 na idadi ya watu milioni 45. Zaidi ya 97% ya watu wa Sudan ni Waislamu.