Iran na nchi tatu za Ulaya zaafikiana kuendeleza mazungumzo ya kidiplomasia
Nov 30, 2024 07:28 UTC
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran wa masuala ya Sheria na Kimataifa amesema Jamhuri ya Kiislamu na nchi tatu za Ulaya zimeafikiana kuendeleza mazungumzo ya kidiplomasia.
Kazem Gharib Abadi, ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X: "duru nyingine ya mazungumzo imefanyika na wakurugenzi wa kisiasa wa Ufaransa, Ujerumani na Uingereza, na matukio ya hivi karibuni ya baina ya pande mbili, ya kieneo na kimataifa hususan masuala ya nyuklia na kuondolewa vikwazo, yalijadiliwa na kutathminiwa.
Gharib Abadi amesema: "sisi tumejizatiti kwa uthabiti kufuatilia maslahi ya wananchi wa Iran, na tunafadhilisha kutumia njia ya mazungumzo na maelewano".
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, katika mkutano huo, iliafikiwa kwambaa mazungumzo ya kidiplomasia yataendelea katika siku chache zijazo.
Kabla ya hapo Ismail Baqaei Hamaneh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alizungumzia sera ya msingi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kuwa na maelewano na mashirikiano na nchi zingine kwa kuzingatia misingi ya heshima, hekima na maslahi, na akabainisha kuwa mazungumzo hayo na nchi tatu za Ulaya ni mwendelezo wa mazungumzo yaliyofanyika pembeni ya mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliofanyika mjini New York.../
Tags