Ismail Baqaei: Utambulisho na malengo ya magaidi nchini Syria hayajabadilika
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa mienendo ya makundi ya kigaidi ni tofauti na zamani, lakini kwamba utambulisho na malengo yao hayajabadilika.
Akizungumza leo katika mkutano wa kila wiki na vyombo vya habari hapa mjini Tehran, Ismail Baqaei ameashiria matukio ya kigaidi huko Syria na kusema: Mienendo ya makundi ya kigaidi ni tofauti na zamani, lakini asili na malengo yao hayajabadilika na fikra zao ni zile zile.
Baqaei ameitaja hali tete ya matukio ya Syria kuwa ni natija ya kudumu kwa muda mrefu mgogoro nchini humo na kusema lengo la utawala wa Kizayuni la kuwaunga mkono magaidi ni kuibua machafuko katika eneo na fitna kati ya nchi za Kiislamu; lakini mara hii nchi za Kiislamu zipo macho na ule udharura wa kuwa na lugha ya pamoja kwa ajili ya kukabiliana na hatari ya ugaidi unadhihirika zaidi hivi sasa kuliko huko nyuma.
Msemaji wa chombo cha diplomasia cha Iran ameongeza kuwa: Kujiri kwa wakati mmoja usitishaji vita huko Lebanon na viongozi wa Marekani kusema kuwa hakuna hatari yoyote kwa Marekani kutoka kwa magaidi kunaonyesha ushirikiano uliopo kati ya magaidi hao na Israel pamoja na Marekani katika kushadidisha mgogoro huko Syria.
Akiendelea na mkutano na waandishi wa habari, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa sera za nyuklia za Iran zinaendea kuwa imara na miradi ya nyuklia ya Iran inafanyika kwa malengo ya amani. "Iran siku zote inajaribu kuzia mivutano katika miradi yake ya nyuklia," amesema Ismail Baqaei.